Wanachuo wajitetea kuchukua Sh180 badala ya karamu ya Sh1m kutoka kwa zawadi ya Rais
MARGARET KIMATHI na CHARLES WASONGA
MNAMO Jumanne Aprili 9, 2024, Wakenya walitumia majukwaa mbalimbali mitandaoni kuhoji Sh180 zilizogawiwa kila mwanafunzi baada ya Rais William Ruto kupeana Sh1 milioni kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi.
Waliuliza ni sababu gani wanafunzi hao kuamua wagawiwe pesa hizo badala ya kutumika kuwaandaliwa chakula.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo, wanafunzi walichukulia Sh180 kama “pesa nyingi” ambazo wanaweza kutumia kununua chakula kwa wiki moja, badala ya dhifa ya chakula cha siku moja.
“Huwa tunatumia Sh25 kununua chakula cha mchana na hivyo nikiwa na Sh180 ninaweza kula kwa siku saba. Pesa hizo pia zitanisaidia kwa mahitaji mbalimbali kwa sababu wazazi mara nyingi huchelewa kutuma pesa za matumizi,” akasema Lewis Murimu, anayesomea taaluma ya uhandisi wa stima.
Akaongeza: “Pesa mkononi ni bora kwa sababu sio kila mtu atafaidi kwa chakula hicho cha siku moja. Kwa hivyo, niliunga mkono wazo kwamba pesa hizo zigawanywe kwa usawa ili kila mtu aridhike kuwa ametendewa haki.
Murimu alisema kuwa alikuwa amekwisha kufanya hesabu zake kabla ya kupigia kura uamuzi huo.
“Nilipiga hesabu na kubaini kuwa kila mwanafunzi atapokea Sh150 lakini ikatokea tungepokea pesa zaidi,” akasema.
Kulingana na taarifa iliyotolewa Aprili 9 na Mkurugenzi wa Masilahi ya Wanafunzi Esther Nthiga maoni yaliyokusanywa kwa njia ya mtandaoni yalionyesha kuwa wanafunzi wengi walitaka zawadi hiyo igawanywe kwa usawa.
Wanafunzi walipewa chaguo tatu kuhusu namna ya kufaidi kwa zawadi hiyo; kugawana pesa hizo kwa njia sawa, kuandaa dhifa ya chakula au kuzipeleka kwa hazina ya basari ya wanafunzi kutoka jamii masikini.
Matokeo ya upigaji kura, kulingana na Nthiga ilikuwa kwamba wanafunzi waliounga mkono pendekezo kwamba pesa hizo zigawanywe walikuwa asilimia 51.
Asilimia 36.4 ya wanafunzi walipendekeza karamu ilhali asilimia 35.5 walitaka pesa hizo zielekezwe kwa hazina ya basari.
Baada ya pendekezo la wengi kushinda na uamuzi wa walioshindwa kuheshimiwa, usimamizi wa chuo hicho kikuu uliamua kuwa kila mwanafunzi apate mgao wa Sh180 kutoka kwa zawadi hiyo kutoka kwa Rais Ruto.
“Baada ya maoni ya wanafunzi kushirikishwa, iliamuliwa kuwa kila mwanafunzi anayesomea shahada ya digrii ya kwanza wakati wa muhula wa kati ya Januari hadi Aprili, wakiwemo wanafunzi ambao wanafanya mazoezi ya kazi ndani ya chuo wakati wa muhula, wapewe Sh180,” ikasema sehemu ya tangazo hili kutoka kwa afisi ya mkurugenzi wa masilahi ya wanafunzi.