Michezo

Miaka 12! Staa wa zamani Chelsea, Real ampiga teke mkewe msaliti

April 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHRIS ADUNGO

MIAKA 12! Huo ndio muda uliomchukua kiungo wa zamani wa Chelsea na Real Madrid, Geremi Njitap, kugundua kuwa mapacha alioamini amezaa yeye mwenyewe ni watoto wa mume wa zamani wa mkewe, Toukam Fotso Laure Verline.

Kulingana na vyombo vya habari nchini kwao Cameroon, Njitap, 45, tayari amewasilisha kesi ya talaka mahakamani baada ya vipimo vya jeni (DNA) kuthibitisha hana unasaba wowote na watoto hao.

“Hakuna watoto wowote wamewahi kuzaliwa katika ndoa au uhusiano wa kimapenzi kati ya Njitap na Toukam,” nyaraka za korti zinasema.

Nyota huyo wa zamani wa Indomitable Lions alifunga pingu za maisha na Toukam miaka minne baada ya mapacha hao kuzaliwa.

Inasemekana alidai watoto hao, waliozaliwa Juni 2008, walikuwa wake na jambo hilo likamchochea hata zaidi kurasimisha uhusiano wake wa kimapenzi na Toukam.

“Lakini ugunduzi kwamba ni wa dume lililotangulia kuchovya asali ya Toukam, umevuruga ndoa yao,” stakabadhi za talaka zinaeleza.

Sasa ameomba uhusiano huo usambaratishwe kirasmi kortini. Jambo hilo limemletea mshtuko mkubwa na msongo wa mawazo,” stakabadhi za talaka zinaeleza.

Hadi vipimo vya DNA vilipofanyika, Njitap alikuwa akiwalea mapacha hao kama watoto wake mwenyewe.

Sogora huyo alichezea Real kati ya Julai 1999 na Julai 2003 kabla kujiunga na Chelsea inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Aliwahi pia kuvalia jezi za Middlesbrough kwa mkopo kati ya Julai 2002 na Mei 2003 kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Chelsea waliojivunia maarifa yake hadi Julai 2007 ambapo walimwachilia kuyoyomea Newcastle United akiwa mchezaji huru.

Aliagana na Newcastle mnamo Julai 2010 na kuelekea Uturuki alikovalia jezi za Ankaragucu kwa miezi saba kabla ya kutua Ugiriki ambapo alichezea AE Larisa hadi alipostaafu soka mnamo Januari 2011.