Kama mna nguvu mtufikie basi, Man City waashiria Arsenal na Liverpool wakilipua Luton 5-1
Na GEOFFREY ANENE
MABINGWA watetezi Manchester City wameng’oa Arsenal kileleni mwa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kukung’uta Luton Town 5-1 ugani Etihad, Jumamosi.
City, ambao hawajapoteza michuano 41 sasa nyumbani katika mashindano yote, walipata bao la kwanza kupitia beki Daiki Hashioka aliyejifunga dakika ya pili baada ya shuti la Erling Haaland kumgusa na kujaa wavuni.
City walifanya maangamizi makubwa katika kipindi cha pili kupitia mabao ya Mateo Kovacic dakika ya 64), Haaland (penalti dakika ya 76), Jeremy Doku (87) na Josko Gvardiol (90+3).
Winga matata Doku alikuwa mwiba kwa Luton katika mchuano huo akichangia pia katika kuzalishwa kwa goli lililofungwa na Gvardiol. Ross Barkely alipachika bao la Luton kujifariji dakika ya 81.
City walikuwa wamezoa ushindi mara nne mfululizo nyumbani dhidi ya Luton kwa jumla ya mabao 12-1. Ushindi mbichi unamaanisha kuwa vijana wa kocha Pep Guardiola wana pointi 73 kutokana na mechi 32. Wako mbele ya nambari mbili Arsenal na nambari tatu Liverpool kwa alama mbili.
Arsenal na Liverpool watasakata mechi yao ya 32 hapo Jumapili wakati vijana wa kocha Mikel Arteta wataalika Aston Villa (nambari nne) ugani Emirates nao Liverpool ya kocha Jurgen Klopp pia iko nyumbani dhidi ya Crystal Palace (nambari 15) ugani Anfield.
Katika michuano mingine imesakatwa Jumamosi, wenyeji Nottingham Forest wametoka 2-2 dhidi ya Wolves, Burnley wakagawana alama na wageni Brighton katika sare ya 1-1, wenyeji Brentford wakazima Sheffield United 2-0 nao Newcastle United wakatumia uga wao wa nyumbani wa St James’ Park kulipua Tottenham Hotspur 4-0.
Luton, Burnley na Sheffield wanasalia katika mduara hatari wa kushushwa ngazi wakiwa wamezoa pointi 25, 20 na 16, mtawalia.