Habari za Kitaifa

Washtakiwa kwa ulaghai wa shamba la Sh14 bilioni

April 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MAAFISA watatu wa kampuni ya kununua mashamba ya Aimi Ma Lukenya Society (AML) wameshtakiwa kwa unyakuzi wa shamba la ekari 4,298 ya kampuni ya kutengeneza saruji ya East African Portland Cement Company (EAPC) lenye thamani ya Sh14.1 bilioni.

Mabw Julius Mutie Mutua, Pascal Kiseli na Alex Kyalo Mutemi walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bernard Ochoi.

Watatu hao walikana mashtaka 24 ya kula njama kulaghai EAPC shamba lake la ekari 4,298 lenye thamani ya Sh14.1 bilioni.

Washtakiwa hao walikana kupunja wawekezaji kima cha zaidi ya Sh25 milioni kwa kuwauzia vipande vya ardhi hiyo ya EAPC wakidai shamba hilo lilikuwa lao.

Bw Ochoi alielezwa kwamba mnamo Septemba 2023 majumba ya kifahari yaliyokuwa yamejengwa kwenye ardhi hiyo yalibomolewa.

Mabw Mutua, Kiseli na Mutemi kupitia kwa mawakili wao Joseph Mutava na Jackson Kala waliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana wakisema “hawatatoroka na watafika kortini kila wanapohitajika.”

Walieleza hakimu kuwa wanaugua maradhi yanayohitaji matumizi ya dawa kila mara pamoja na kukaguliwa na daktari.

Bw Mutava alieleza hakimu kwamba washtakiwa hao walitiwa nguvuni Oktoba 19, 2023 na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh100, 000 na hakimu mwandamizi Gilbert Shikwe,

“Washtakiwa hawa wamekuwa wakifika kortini kila mara kwa miezi hiyo saba iliyopita,” Bw Mutava alimweleza Hakimu Ochoi.

Pia mahakama ilifahamishwa kesi ya mmiliki halisi wa shamba hilo inaendelea katika Mahakama ya Rufaa.

“Ni kinyume cha sheria na utumizi mbaya wa mahakama mmoja kukamatwa na kushtakiwa wakati kuna kesi inayoendelea katika Mahakama ya Rufaa kuhusu umiliki wa shamba hili,” alisema Bw Mutava.

Alisema Mabw Mutua, Kiseli na Mutemi wana hati ya umiliki wa shamba hilo na “kile wanachojua shamba hilo ni la wanachama 10,000 wa AML na wala sio la kiwanda hicho cha saruji.”

Mahakama iliombwa iwaachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu.

Kiongozi wa mashtaka James Gachoka hakupinga ombi la watatu hao kuachiliwa kwa dhamana, ila aliomba mahakama izingatie uzito wa mashtaka yanayowakabili.

Katika uamuzi wake, Bw Ochoi alisema washtakiwa wamezua suala la kuwa ni wagonjwa lakini hawakuwasilisha ripoti yoyote ya hospitali wanakoenda kutibiwa.

Aliamuru idara ya urekebishaji tabia iwahoji washtakiwa pamoja na watu wa familia zao kuhusu hali zao za kiafya.

Bw Ochoi aliagiza washtakiwa wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Capitol Hill hadi Aprili 15, 2024 atakapoamua hatma yao ya dhamana.