Nyota ya Liverpool EPL yazimwa 1-0 na Crystal Palace
NA MWANGI MUIRURI
LIVERPOOL imesimamishwa na Crystal Palace katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kutandikwa bao moja kwa nunge.
Mtanange huo wa Aprili 14, 2023 ugani Anfield – nyumbani kwa Liverpool, ulipata goli hilo la maangamizi kupitia sogora Eberechi Oluchi Eze wa miaka 25, raia wa Uingereza kunako dakika ya 14.
Ni goli lililotiwa kimyani kupitia ufundi mkuu wa ushirikiano kiasi kwamba licha ya kuumizwa, kocha wa Liverpool Jurgen Klopp alionekana wazi akishabikia kwa kutamka neno “wow“.
Huku mchongoano mitandaoni ukisema kwamba Liverpool imeanza kukoma kuwa farasi katika mbio za ubingwa na kuchukua sura ya kihongwe, wadadisi wanakubaliana kwamba ni mechi ilikataa vijana hao wa Klopp.
Liverpool ilitamalaki mchezo huo kwa umiliki wa mpira kwa asilimia 70 na kuachilia fataki 21 dhidi ya 8 zile za Crystal Palace.
Kati ya fataki za Liverpool, ni 6 zililenga kimyani lakini bila bahati kusimama huku 5 za Crystal Palace zikizaa goli hilo moja na pointi 3 muhimu katika jedwali.
Kurambwa huko kwa Liverpool kumezidisha presha katika jedwali ambalo kwa sasa linaongozwa na Man City kwa pointi 73 huku Arsenal iliyo ya pili ikiwa na pointi 71 ilianza kuvaana na Aston Villa saa kumi na mbili na nusu (Jumapili, Aprili 14, 2024).
Ushindi utairusha kileleni kwa pointi 74, droo iiache katika nafasi ya pili kwa pointi 72 na ikipoteza ibaki tu katika nafasi hiyo ya pili.
Liverpool ni ya tatu kwa pointi 71 japo ikidunishwa kwa mabao na Arsenal.
Huku ligi ikibakia mechi 6 (pointi 18) ikamilike, mkabano huo mkali kati ya timu hizo tatu umekuwa wa kusisimua mashabiki wa soka huku wafuasi wakikaza kukaza.