Makala

Safari ya Mkenya anayemiliki hospitali Amerika 

April 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA PETER CHANGTOEK

CHRISTINE Ouma alisafiri Amerika 2001, alipokuwa na umri wa miaka 20.

Kwa sasa anamiliki hospitali katika jimbo la Texas, nchini Amerika.

Alisomea taaluma ya uuguzi katika chuo cha Houston Community College kilichoko Houston TX, ambapo alikabidhiwa cheti cha LVN mwaka 2008 na kusajiliwa pia katika taasisi ya Excelsior College, Albany, New York, mwaka 2020.

“Jina langu rasmi la usajili ni RN CRNI®, kwa hivyo, hujulikana kama Christine Ouma RN CRNI®,” akafichua kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Dijitali.

Aliasisi kampuni yake ya kutoa huduma za afya 2018, lakini wakati huo, alikuwa akifanya kazi kwingine, na akaitumia kama mbinu ya kupata mapato ya ziada.

Aliacha kazi hiyo Juni 2022, na kujitosa kikamilifu katika utoaji huduma za uuguzi katika kampuni yake inayojulikana kwa jina Healing Bridges Infusion Specialists, ambapo hutoa huduma katika maeneo tofauti tofauti, kama vile nyumbani kwa wagonjwa, vituo vya huduma katika afisi za madaktari, na katika maeneo yanayouza dawa.

“Kilichonitia motisha ni mapenzi yangu kwa uuguzi wa kunywesha dawa, na mwito wa kutoa huduma,” asema muuguzi huyo.

“Niliamua kuhudumu hapa kwa sababu Amerika ni nyumbani kwa sasa, na nina kibali cha kuhudumu. Pia, ni rahisi kwangu kama muuguzi kumiliki biashara hii katika nchi hii, kwa sababu sheria na mwongozo, itifaki na miundo, hata kama ni kali, zimebuniwa, kufanyiwa utafiti, kuandikwa; kwa hivyo, ni salama kuwa mhudumu wa kujitegemea,” aeleza.

Muuguzi huyu hutoa huduma za uuguzi katika maeneo ya Houston, TX na miji mingine iliyoko karibu na maeneo hayo.

Anasema kwamba, shughuli hiyo ni ghali kuanzisha, kwa sababu kuna leseni na stakabadhi ambazo zinafaa kutolewa katika jimbo la Texas, ambazo ni sharti muuguzi awe nazo, kabla hajamgusa mgonjwa.

Ouma anasema kuwa, baada ya kufanya kazi saba za kuajiriwa ambazo hazikumfurahisha kwa muda wa mwaka mmoja, alipata kazi ya uuguzi wa kunywesha dawa kwa bahati tu.

“Haikuwa kwa uwezo wangu. Nilifika hapa kwa neema ya Mungu; nikaipenda, nikakwamilia na kuwa bora kwayo, na hapa ndipo tupo sasa,” asema.

Muuguzi huyo anafichua kuwa, alianza shughuli hiyo peke yake, kama mhudumu, na alikuwa akiwaalika wauguzi wenzake kumsaidia wakati alipokuwa akisafiri, na wakawa timu moja pamoja.

Kwa sasa, ana wafanyakazi zaidi ya kumi – watatu wanaoshughulika afisini na wengine wanaohudumia wagonjwa nje ya afisi.

Ouma anasema kuwa, wauguzi wanapoenda kuwashughulikia wagonjwa nyumbani, humhudumia mgonjwa mmoja kwa wakati mmoja, lakini wagonjwa wanapotembelea kituo chao cha matibabu, muuguzi mmoja huwahudumia wagonjwa watatu au zaidi, kila mmoja, kwa wakati mmoja.

Anadokeza kuwa, baadhi ya wagonjwa huhudumiwa kwa muda wa dakika 15 tu.

Anaongeza kuwa, kuna mambo fulani yanayochangia idadi ya wagonjwa wanaoshughulikiwa.

Muuguzi huyo anasema kwamba, anapania kupanua biashara hiyo ili kuwahudumia wagonjwa wengi katika eneo la Texas, na katika maeneo mengine yaliyoko Amerika.