Makala

Huzuni chifu akijitia kitanzi barabarani

April 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

HALI ya majonzi imetanda katika eneobunge la Gatundu Kaskazini baada ya chifu wa eneo la Gituamba kujitia kitanzia katika Kaunti ya Murang’a.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi kuhusu kisa hicho, Bw Stephen Ng’ang’a ambaye ni Naibu wa Chifu wa Kata ya Gituamba alipatikana Aprili 12, 2024 akiwa amejinyonga kwa kamba karibu na shamba la mananasi la Del Monte.

Wapitanjia waliouona mwili wake walipiga simu kwa maafisa wa polisi ambao walifika eneo hilo na kuupeleka hadi Mochari ya General Kago kuhifadhiwa, uchunguzi ukiendelea.

“Mwili wake ulikuwa unaning’inia kwenye mti ulio karibu na eneo la Del View. Baada ya uchunguzi wa eneo la mkasa kutekelezwa, mwili ulitambuliwa kutokana na stakabadhi zilizokuwa ndani ya mkoba kando yake,” ripoti hiyo ya polisi yasema.

Alikuwa na kamba shingoni, iliyofungwa kwenye tawi la mti.

Taarifa ya polisi inaarifu kwamba familia ya marehemu ilifahamishwa na ikafika kuutambua mwili.

Kwa sasa, dhana kuu ni ilikuwa mauti ya kujitoa uhai kimakusudi.

Kwenye stakabadhi zilizotwaliwa, karatasi yenye ujumbe ilipotikana inayosema aliafikia uamuzi huo kutokana na msongo wa mawazo.

Alikuwa amewaelekeza majirani kadha na pia mkubwa wake ambaye ni msaidizi wa Naibu Kamishna wahakikishe kwamba watoto wake hawatahangaika.

Msemaji wa familia ya mwendazake, Bw Simon Kariuki alisema kwamba “tumehuzunika kwa kuwa mwendazake alikuwa akitumia dawa za kuzima mawazo lakini alivyosafiri kutoka nyumbani na kuishia kujiua katika barabara ya Thika kuelekea Kenol, ni kizungumkuti”.

Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bw Elijah Kururia aliteta kwamba visa vya watu kujitoa uhai vimezidi huku akiomba jamaa na marafiki katika jamii wawe wakitoa ushauri nasaha kwa wapendwa wao walioathirika.

“Ni vyema tuwe walezi katika jamii kwa wagonjwa wa msongo wa mawazo. Tunaposhuku kwamba mmoja wetu ameathirika, tunafaa kuwajibikia suala hilo na kusaka usaidizi hata wa kimatibabu kabla ya hali kugeuka kuwa janga,” akasema.

Bw Kururia alisema kwamba atashirikiana na familia ya marehemu kwa hali na mali.

Mbunge Mwakilishi Kaunti ya Kiambu, Bi Anne Wa Muratha alisema kwamba “nilikuwa nimetoa onyo la mapema kwamba jamii imeathirika vibaya katika janga la msongo wa mawazo lakini nikaeleweka visivyo, kwa sasa imedhihirika tuna shida kubwa”.

Katika kampeni za uwaniaji uchaguzi mkuu wa 2022, Bi Muratha alisema kwamba iwapo angeshinda wadhifa huo basi angetilia maanani utatuzi wa shida za kimawazo lakini kwa mitandao akasutwa kwa kiwango kikuu kwamba alisema “Kaunti ya Kiambu imejaa wendawazimu”.

[email protected]