Spika wa Nairobi mashakani kwa ‘kulazimisha’ salamu na mwanamke Muislamu
NA NDUBI MOTURI
SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Ken Ng’ondi amejikuta mashakani baada ya video kufichuka ikimuonyesha ‘akimlazimisha’ mwanamke Muislamu kumsalimia wakati wa sherehe ya bethidei.
Kwenye video hiyo ambayo Taifa Leo imeona, Bw Ng’ondi anaonekana akisalimia na kupiga pambaja wageni kisha anamfikia mwanamke mmoja aliyekaa.
Licha ya kwamba mwanamke huyo aliyevalia buibui kukataa kushika mkono wake, Spika huyo anamlazimisha na kumsimamisha kwa nguvu na kumpiga pambaja huku akimwambia mpiga awapige picha.
“Nisalimie leo! Ni sikukuu yangu ya kuzaliwa!” Bw Ng’ondi anasikika akiambia mwanamke huyo.
Mwanamke huyo hata hivyo anakataa kufuatwafuatwa huko kabla kulazimishwa kusimama.
Wanaume wengine wanamshangilia spika wakimtaka mwanamke huyo kupeana salamu.
Video hiyo ilichukuliwa wakati wa sherehe ya bethidei katika Bunge la Kaunti ya Nairobi Novemba 23, 2022 punde baada ya Uchaguzi Mkuu.
Baada ya kusambazwa mitandaoni, viongozi wa Kiislamu wameelezea kugadhabishwa kwao na kitendo hicho na kutaka spika huyo ajiuzulu wakisema alimnyanyasa mwanamke huyo kimapenzi.
Shirikisho la Mawakili wa Kike limemtaka Bw Ng’ondi afunguliwe mashtaka ya unyanyasaji wa kimapenzi.
“Kitendo cha aibu, na kinyume cha sheria. Hakikiuki pekee mila za kidini bali pia zinaingilia uhuru wa kimwili wa mtu binafsi. Kwa hivyo tunataka uwajibikaji na mashtaka ya kihalifu yafunguliwe mara moja na DCI dhidi ya Bw Ken Ng’ondi kwa kosa hili bovu,” taarifa ya shirikisho hilo ikasema.