Habari za Kitaifa

Mmiliki wa kilabu, wafanyakazi wake wapatikana na hatia ya kumuua mbunge wa zamani George Thuo

April 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa Porkies Club Paul Wainaina Boiyo na wafanyakazi wake watano wamepatikana na hatia ya kumuua aliyekuwa Mbunge wa Juja George Thuo miaka 11 iliyopita.

Lakini punde tu Jaji  Roselyn Korir alipotoa uamuzi huo mkongwe Dkt John Khaminwa alimweleza amemshtua sawia na washtakiwa.

Ulikuwa mwendo wa saa tisa na robo Jaji Korir aliposoma uamuzi kwamba Boiyo na wafanyakazi wake watano ndio walimuua Thuo kwa kumtilia sumu kwenye pombe sumu iliyochoma viungo kwenye utumbo wake.

Jaji Korir aliwapata na hatia Boiyo, Christopher Lumbasio Andika, Andrew Karanja Wainaina, Samuel Kuria Ngugi, Esther Ndinda Mulinge na Ruth Vanessa Irungu ya kumuua Thuo, Dkt Khaminwa alisema “sikubaliani nawe. Umenishtua mno. Nitapinga uamuzi huu Mahakama ya Juu.”

Jaji Korir aliwapata na hatia sita hao kwa mauaji ya Thuo yaliyofanyika Novemba 19, 2013.

Dkt Khaminwa alimweleza Jaji Korir kwa mshangao, “Uamuzi huu wako umenishtua sana. Sikutarajia utawapata na hatia washtakiwa.Haiwezekani watu sita wamnyweshe sumu mtu mmoja.”

Jaji Korir alichambua ushahidi dhidi ya kila mmoja na kusema Vanessa alimnunulia bia Thuo kisha “akamkumbatia na kumbusu baada ya kumkabidhi chupa.”

Hata hivyo Dkt Khaminwa aliomba washtakiwa waachiliwe kwa dhamana wakisubiri kuhukumiwa mnamo Mei 3, 2024.

Na wakati huo huo Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Igonga aliomba idara ya urekebishaji tabia iwahoji washtakiwa na familia ya marehemu kabla ya adhabu kupitishwa.

Akitathmini ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, Jaji Korir alisema “washtakiwa wote walihusika kwa njia moja au nyingine katika kifo cha Thuo ambaye Dkt Khaminwa na mawakili wengine walisema alikuwa anahofia maisha yake.”

Thuo alikuwa atoe ushahidi mjini The Hague

Jaji Korir alisema Thuo alikuwa ameorodhesha kutoa ushahidi katika mahakama ya uhalifu ya kimataifa (ICC) yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi.

Rais William Ruto na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta walikuwa wameshtakiwa kwa kudaiwa kushiriki katika ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 ambapo watu zaidi ya 1,000 walikufa na wengine zaidi ya 600,000 kuhamishwa makwao.

Mawakili waliowatetea washtakiwa hao walisema huenda waliomtishia maisha Thuo ndio waliohusika.

Lakini Jaji Korir alitupilia mbali tetezi na kusema washtakiwa ndio walihusika na kutia sumu katika pombe Thuo alimimina siku hiyo akitazama mchezo wa Formula One kwenye kilabu.

Mahakama ilisema Thuo aliaga kutokana na kuvuja damu kwenye utumbo wake na machengelele.

“Boiyo na Andika walikuwa wamezugumza na Thuo kabla ya kutoka kwa nyumba yake. Wawili hao walikuwa na muda wa kutosha kumpangia hila au wema mwanasiasa huyo,” Jaji Korir alisema.

Aliongeza kusema wafanyakazi wawili wa Boiyo waliketi naye kwenye meza moja na hawakutoka muda huo wote hadi pale Thuo alipoanguka na kuzirai.

Kabla ya kuzirai alikuwa amemweleza Boiyo kwamba anahisi joto kisha akaenda kutoa vesti ndani ya afisi yake na kuipeleka kwenye gari lake.

Alipofika kwenye kilabu aliuziwa pombe na Ndinda na ukaguzi uliofanyiwa chupa za pombe na gilasi zilikutwa na sumu ambayo ilimuua Thuo.

Jaji huyo alisema Vanessa alimnunulia pombe Thuo kisha akamkumbatia na kumbusu hata mahakama ikashangaa “je busu hilo lilikuwa la kumsaliti jinsi Judas Iscariot alivyombusu Yesu kabla ya kukamatwa na hatimaye kusulubiwa.”

Jaji huyo aliamuru idara ya  urekebishaji tabia iwahoji washtakiwa na mlalamishi kisha iwasilishe ripoti kortini Mei 3 kabla ta hukumu kupitishwa.