Jenerali Ogolla alikufa akitekeleza agizo la Ruto
JENERALI Francis Ogolla aliyefariki dunia katika ajali ya helikopta Alhamisi alikuwa katika ziara ya kutekeleza agizo la Rais William Ruto kwamba wanajeshi wafike katika shule ambazo zimeathirika na ujangili kuzikarabati.
Rais alitoa agizo hilo alipofungua kiwanda cha simiti katika Kaunti ya Pokot Magharibi mnamo Aprili 8.
Taifa Leo imebaini kuwa Jenerali Ogolla alikuwa anaharakisha kazi hiyo imalizike kwa wakati unaotakikana.
Kikosi cha wanajeshi kilifika katika shule hizo kwa muda uliotakiwa.
Hata hivyo, Mkuu wa Majeshi na wanajeshi wengine 9 walifariki wakiwa kazini eneo la Sindar, Kaben, Kaunti ya Elgeyo Marakwet dakika chache baada ya kuondoka shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel katika Kaunti ya Pokot Magharibi.
Shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel inayopatikana Chesegon kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na –Elgeyo Marakwet na ambayo Jenerali Ogolla alizuru mwisho kabla ya kukutana na mauti haina wanafunzi.
Wanafunzi wa shule hiyo wako katika shule ya msingi ya Surumben wadi ya Masol umbali wa kilomita 50 kutoka eneo hilo.
James Koitilo, mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Cheptulel Boys alisema kuwa hakuna maji kwenye shule hiyo baada ya bomba kuharibiwa, jikoni kuangushwa, nyumba za walimu kuharibiwa na mabati kung’olewa na majangili.
Jenerali Ogolla ambaye aliweka saini kwenye kitabu cha wageni katika shule hiyo aliwataka wazazi ambao walikuwepo kurudisha wanao shuleni baada ya shule hizo kukarabatiwa.
Jenerali Ogolla pia alizungumza na watoto watatu katika shule hiyo ya Cheptulel ambao walikuwa wamevaa nguo za kawaida. Aliwahimiza kufanya bidii shuleni.
Watoto hao wanatoka shule ambazo ziliathirika na ujangili katika eneo hilo.
Zaidi ya shule 50 zimeathiriwa na visa vya ujangili eneo la Kaskazini mwa Bonde la ufa.