Makala

‘Ufisadi wa polisi, kanjo utaponza Thika kuwa jiji’

April 22nd, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

WADAU wameambia Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi kwamba mahasla wanafaa wakubaliwe kuvumisha biashara zao pasipo kero nyingi ambazo hutokana na misako ya polisi na askari wa kaunti almaarufu ‘kanjo’.

Mshirikishi wa muungano wa wafanyabiashara wa kiwango cha chini mjini humo Bi Anne Wambui aliteta kwamba mahasla mjini Thika huhangaishwa sana na maafisa hao.

Vibiritingoma nao wameungana na mahasla wengine kumtaka Bw Wamatangi azingatie masilahi yao anaposaka hadhi ya mji huo kuwa jiji.

Wamehofia kwamba mikakati ya mahasla kufurushwa ili kupisha matajiri kuthibiti mji huo itazinduliwa punde tu hadhi ya jiji itafanikishwa.

Mnamo Aprili 12, 2024, gavana alitangaza kuundwa kwa kamati maalum ya kufanikisha msukumo huo akisema kwamba tayari ni mpango ambao umechelewa.

“Kuchelewa huko kwa Thika kuwa Jiji kumetokana na siasa mbaya ambazo hadi sasa zimetupokonya uwezo wa kupata ufathili wa Sh1 bilioni kutoka kwa mashirika kadha. Kwa sasa tunafaa tujizatiti ili mpango huu ufanikiwe kwa kuwa utakuwa wa manufaa kwa wadau wote,” akasema.

Hata hivyo, makahaba wameingiwa na wasiwasi wakisema kwamba Mahasla wanafaa wakubaliwe kuvumisha  biashara zao pasipo kero nyingi ambazo hutokana na misako ya polisi na kanjo.

Mshirikishi wa muungano wa wafanyabiashara wa kiwango cha chini mjini humo Bi Anne Wambui aliteta kwamba mahasla mjini Thika huhangaishwa sana na polisi na pia kanjo.

“Kando na hao wanawake wa kujiuza kimwili, sisi wengine hukumbana na misako ya kuvumisha ufisadi miongoni mwa maafisa kadha wa kituo cha polisi cha Thika na pia askari wa serikali ya kaunti ya Kiambu,” Bi Wambui akasema.

Alisema kwamba wamekuwa wakilalamika kwa ofisi husika lakini hakuna afueni wao hupata, akiongeza kwamba maafisa hao wafisadi wameunda magenge ya wahuni wa kuwasaidia kukusanya hongo kutoka kwa makahaba.

“Maafisa hao huzunguka huku wakitafuta wa kuitisha pesa za hongo hata weakati hakuna makosa. Mimi nimeshuhudia maafisa wa polisi wakiwadai Sh100 wanawake hao wa kujiuza kimwili ili wasikamatwe. Kanjo nao huwadai Sh50. Katika biashara nyingine tunaitishwa kati ya Sh200 na Sh1000 kama hongo.  Ni serikali iliyo na ujambazi mwingi sana,” akasema.

Ni masuala nyeti ambayo Taifa Leo ilifahamishwa na wadokezi kwamba kamati ya masuala ya usalama ya Kaunti ya Kiambu inawajibikia baada ya kufahamishwa.

“Tuko na habari hizo na tumezinakili kama hali za dharura ambazo ni KIA9545178 na KIA4462169. Maafisa wa kiusalama wanaangalia hali hizo,” akasema mdokezi wetu.

Bi Wambui alisema maafisa hao wadhalimu wa polisi na kanjo wanafaa kuzimwa ili waache kuua mianya ya kujipa riziki.

Hata hivyo, kisheria ni hatia kuchuuza mahaba lakini wakili Geoffrey Kahuthu wa Mahakama Kuu, anashikilia kwamba hakuna hatia inayoweza ikathibitika kortini bora tu mshtakiwa asikiri mashtaka yakisomwa.

“Hakuna vile unaweza ukathibitisha watu wawili wa jinsia tofauti na walio na umri wa miaka 18 kwenda juu wakiwa kwa mahaba ya hiari kwamba walikuwa wakishiriki ukahaba,” akasema.

Alisema kwamba wanaodaiwa hongo kwa msingi wa kuwa katika biashara haramu wanafaa kukaidi na wazidishe kelele za kukemea ufisadi huo.

Mwenyekiti wa muungano wa wafanyabiashara wa Thika Bw Alfred Wanyoike akiwa katika kikao na waandishi wa habari Aprili 12, 2024, aliteta kwamba “usumbufu wa kanjo umezidi katika mji huo”.

Alisema kwamba misako kiholela na baadhi yao kunyang’anywa bidhaa za uchuuzi hufanya wadau kujiuliza kama hadhi ya Thika kuwa Jiji itawafaa.