Habari za Kaunti

Hofu baada ya wanne kujeruhiwa na mifugo kuzikwa kwenye maporomoko ya tope

April 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA OSCAR KAKAI

CHEPURAI Ng’oletiang, mwenye umri wa miaka 45, mama wa watoto watano alikuwa kwenye shughuli ya kuandaa chamcha majira ya sita mchana kwenye nyumba yake katika kijiji cha Kaptaram, Lokesheni ya Kopro, kaunti ndogo ya Pokot ya Kati, Kaunti ya Pokot Magharibi.

Ghafla bin vuu, alisikia sauti ya kutisha na nduru ya ajabu kutoka nje. Alitoka upesi na kuona mawe na udongo kwenye mlima wa Kokotendwo yakiporomoka, umbali wa kilomita tatu.

Kusonga karibu, aliona watu wamefunikwa kwenye mchanga. Alipigwa na butwa hali ambayo ilipelekea ugonjwa wake wa presha kurejea.

Bi Chepurai ambaye anapokea matibabu katika hospitali ya kaunti ya rufaa ya Kapenguria na wanne wengine ambao walijeruhiwa anasema kuwa hali hiyo ilikuwa mbaya zaidi.

Tukio hilo lilisababishwa na mvua kubwa inayonyesha eneo hilo tokea Jumamosi na kuwaacha watu wanne wakiwemo akina mama wawili na wazee wawili na majeraha. Mbuzi watatu pia walifunikwa na mchanga kisha wakafariki.

Naibu wa chifu wa Lokesheni ya Kokotendwo Samuel Samut anasema kuwa waathiriwa walikuwa wakichota maji na kutafuta kuni kwenye mlima huo.

Mfugo uliofunikwa na maporomoko ya ardhi katika kijiji cha Kaptaram, Pokot Magharibi. Picha|Oscar Kakai

Anasema kuwa watu wanne walipata majeraha kwenye vichwa, miguu na mikono.

Bw Samut anasema kuwa waathiriwa hao walitibiwa katika zahanati ya Kokotendwo na baadaye kupewa uhamisho hadi hospitali ya rufaa ya kaunti Kapenguria kupata matibabu zaidi.

“Ni mara ya kwanza maporomoko ya tope kufanyika kwenye kijiji hiki. Hata hakukuwa kunanyesha siku hiyo lakinimvua ilikuwemo Ijumaa,” anasema.

Anasema kuwa kisa hicho kimewaweka zaidi ya watu 200 wa kijiji hicho kwenye hatari.

Anasema kuwa amewaambia wakazi ambao wanaishi nyanda za chini ya milima kuhamia maeneo salama.

“Wengine wamepiga kambi katika Shule ya Msingi ya Kokotendwo na wengine wamejiunga na watu wa ukoo wao,” anasema.

Mshirikishi wa shirika la Msalaba Mwekundu Pokot Magharibi Scholasticah Kapello ambaye alizuru eneo hilo Jumamosi anasema kuwa hali hiyo ilikuwa mbaya na wakazi wanahitaji msaada.

Alisema kuwa maporokomo hayo yalitokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.

Mwakilishi wa wadi ya Weiwei David Moiben ambaye alizuru eneo la mkasa alisema kuwa eneo hilo ni la muiniko.

“Wakazi wengi na waathiriwa wanaishi kwenye hofu kuwa maporomoko mengine yatatokea,” anasema.

Mwaka wa 2019, zaidi ya watu 20 walifariki, mali ikaharibiwa na wakazi wakapoteza makao kwenye vijiji vitatu vya Muino, Nyarkulian na Parua baada ya maporomoko ya tope kutokea.

Mmoja wa majeruhi katika mkasa wa maporomoko ya ardhi Pokot Magharibi. Picha|Oscar Kakai

Tukio lingine mbaya lilikuwa la mwaka wa 2020 ambapo watu 50 walipoteza maisha, mali kuharibika, zaidi ya wakazi 1500 kupoteza makao katika eneo la Chesegon baada ya mafuriko na maporomoko ya tope kutokea.

Mwaka jana, mwanamke mmoja aliuawa eneo la Muino, kaunti ndogo ya Pokot ya kati, majengo ya shule ya upili ya Chemutlokotyo kuharibiwa pamoja na soko la Ortum kusombwa na mafuriko.

Maeneo mengine hatari ni Tapach, Sondany, Nyarkulian, Parua, Muino, Cheptongo, Ortum, Kelerwa, Kalee, Solion, maeneo ya juu ya wadi za Batei, Weiwei, Lomut, Cheptulel, Lelan, maeneo ya juu ya Chepareria, Propoi, Reper, Kosilol, mlima wa Mtello, Sakata, Chesegon, Chesta, Solion, Kokotendwo, Karapoy, Kokososion Sondany, Tapach, Batei, Seker na milima ya  Pokot katika kaunti ndogo za Pokot Kusini na kati.

[email protected]