Afya na Jamii

Wito Afrika izinduke kukabiliana na maradhi yasiyo ya kuambukiza

April 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA PAULINE ONGAJI akiwa DAR ES SALAAM, TANZANIA

BARA la Afrika linakodolea macho hatari huku maradhi yasiyo ya kuambukiza yakitabiriwa kusababisha vifo vingi zaidi kufikia mwaka wa 2030.

Haya ni kulingana na Dkt Matsishido Moeti, mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani WHO barani, aliyekuwa akihutubu kupitia mtandao katika kongamano la kwanza kuhusu Mkakati wa PEN-Plus kuangazia maradhi yasiyo ya kuambukiza barani (ICPPA), lilioanza rasmi jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.

Dkt Moeti alisema kwamba maradhi yasiyo ya kuambukiza yamekuwa donda hapa barani, na huenda hali ikawa mbaya hata zaidi hasa ikazingatiwa kwamba mataifa mengi ya Afrika hayawekezi katika kupambana na magonjwa haya.

Alisema kwamba hali ikiendelea hivi, huenda mifumo ya afya hapa barani ambayo tayari inakumbwa na matatizo, ikashindwa kustahimili.

“Takwimu zinaonyesha kwamba mataifa maskini na yale yenye mapato wastani hutumia asilimia 26 katika kutibu maradhi haya, na jinsi mambo yanavyoendelea, huenda hali ikawa mbaya hata zaidi,” aliongeza.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bi Elke Wisch, mwakilishi wa Unicef nchini Tanzania, alisema kwamba ili kushinda vita dhidi ya maradhi yasiyoambukiza, kuna haja ya kutumia teknolojia ili kuhakikisha kwamba huduma za afya zinatolewa na jamii inaahamasishwa.

Shirika la WHO linakadiria kwamba maradhi yasiyoambukiza huua kufikia watu milioni 41 kila mwaka, sawa na asilimia 74 ya vifo duniani, huku wengi wanaoathirika wakiwa kati ya umri wa miaka 30 na 69. Mataifa maskini na yenye mapato wastani, ndio yaliyoathirika pakubwa kwani asilimia 85 ya vifo hivi vinatokea huku.

Aidha, shirika hili laashiria kwamba, katika bara la Afrika ambalo tayari linakumbwa na mzigo mkubwa, maradhi haya yanasababisha asilimia 37 ya vifo, idadi ambayo imeongezeka kutoka asilimia 24, mwaka wa 2000.

Maradhi ya moyo, kisukari, kansa na magonjwa ya mfumo wa kupumua yanawakilisha idadi kubwa ya maradhi yasiyoambukiza barani. Ugonjwa wa moyo husababisha vifo vya watu milioni 17.9 barani kila mwaka, ukifuatiwa na maradhi ya kansa yanayosababisha vifo 9.3 million, huku magonjwa ya mfumo wa kupumua na kisukari, yakisababisha vifo vya watu milioni 4.1 na milioni 1.5 mtawalia.

Kwa upande mwingine, mkakati wa  PEN-Plus ulikubaliwa na mataifa 47 wanachama wa WHO barani, nchini Togo mwaka wa 2022, ambapo unanuia kuangazia mzigo wa maradhi yasiyosambaa hasa miongoni mwa wakazi wa maeneo ya mashambani, kupitia huduma katika vituo vya afya vya mashinani.

Wajumbe katika kongamano la PEN-Plus jijini Dar es Salaam, Tanzania. PICHA | PAULINE ONGAJI

Kulingana na Dkt Yvette Kisaka, mratibu wa mradi wa PEN-Plus katika Wizara ya Afya, kupitia ushirikiano, tayari Kenya inatekeleza mradi huu katika vituo viwili vya afya nchini, huku lengo likiwa kuhakikisha kwamba mradi huu unafikikia sehemu zote nchini kufikia mwaka wa 2030.

“Kupitia mradi wa PEN-Plus inasaidia kutoa huduma kwa wagonjwa  wa maradhi ya selimundu, aina 1 ya kisukari, ugonjwa wa mfumo wa kupumua, magonjwa ya moyo na maradhi ya akili, ambapo tayari matokeo yameanza kushuhudiwa,” aliongeza Dkt Kisaka.

Kila mwaka, takriban watoto 500 nchini Kenya hufariki kutokana na Aina 1 ya kisukari, huku watoto 14,000 wakizaliwa na maradhi ya selimundu. Aidha, zaidi ya Wakenya nusu milioni wameathirika na maradhi ya moyo.

[email protected]