Waliouziwa mbolea feki waanza kulipwa fidia
BARNABAS BII Na KNA
BODI ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) imeanza kuwafidia wakulima waliouziwa mbolea feki.
Mkurugenzi Mkuu wa NCPB, Joseph Kimote, alisema kwamba hatua hiyo inafuatia agizo kutoka kwa Wizara ya Kilimo na Ustawi wa Mifugo kwamba wakulima wote walionunua mbolea iliyosambazwa na kampuni ya KEL walipwe fidia.
“Wakulima wote walioathiriwa wanahimizwa kuwasilisha malalamishi rasmi kwa kujaza fomu ambayo watapatiwa katika depo au vituo vya uuzaji walikonunua mbolea. Pia watatakiwa kutoa kitambulisho cha kitaifa na ithibati kwamba walinunua mbolea,” alieleza Kimote.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema kwamba wakulima wote waliotumia mbolea hiyo na NCPB ilithibitishe ilitoka katika maghala yake watapatiwa mbolea inayotoshana na walionunua kuongezea mimea yao.
“Pale ambapo mkulima aliyenunua mbolea na hakuitumia, atatakiwa kuirudisha kwa maghala ya NCPB na kupatiwa kiasi sawa na walichokuwa wamenunua cha mbolea ya upanzi,” aliongeza Kimote.
Wakati uo huo, Kimote alisema Bodi hiyo imesambaza magunia milioni tatu ya mbolea ya upanzi na 300,000 ya kuongezea mimea msimu huu wa mvua ya masika.
Waliopokea mbolea hiyo ni wakulima waliosajiliwa.Wakulima waliotumia mbolea hiyo wanalalamika kuwa mimea yao imedumaa na wako katika hatari ya kupata hasara.Haya yanajiri huku miito ikiendelea waliohusika na sakata ya mbolea feki wachukuliwe hatua.