Habari za Kitaifa

Kenya Power kulipa Woolworths Sh500m kufidia hasara ya moto Nakumatt

April 24th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini (Kenya Power au KPLC) imeagizwa na Mahakama Kuu ifidie kampuni ya Woolworths, iliyokuwa imekodisha jumba lake kwa Nakumatt Down Town, zaidi ya Sh500 milioni kutokana na moto wa mwaka 2009 ulioteketeza duka lake la Nakumatt Down Town na kusababisha vifo vya watu 30.

Katika uamuzi huo wa kihistoria, Jaji Janet Mong’are alisema kampuni ya KPLC ndio ya kulaumiwa kwa moto huo uliosababisha hasara kuu na kuangamiza maisha ya wafanyakazi na baadhi ya wateja waliokuwa wananunua bidhaa.

Jaji huyo aliondolea kampuni ya Nakumatt Holding Ltd na Mkurugenzi wake mkuu Atulkumar Maganlala Shah lawama kwamba moto huo ulisababishwa na mtambo wake wa jenereta.

Jaji Mong’are alisema ushahidi uliowasilishwa mbele yake kuhusu moto huo wa Januari 29, 2009, ulithibitisha kabisa mtambo wa transfoma wa Kenya Power unaosambaza nishati hadi kwa kampuni ya Nation Media Group ndio ulikuwa na dosari.

Alisema baada ya stima kukatika na kurejeshwa, moto ulilipuka katika duka hilo na kuunguza bidhaa na kuteketeza watu 30.

“Baada ya kutathmini ushahidi wa wafanyakazi wa KPLC Ngei Ntambo na Charles Muhoro, ni bayana moto ulisababishwa na transfoma iliyokuwa na dosari,” alisema Jaji.

Mahakama ilisema Ngei na Muhoro walitofautiana katika ushahidi waliotoa mbele ya mahakama kuhusu chanzo cha moto huo.

Muhoro alieleza mahakama kwamba transfoma iliyokuwa inasambaza nishati (stima) ilikuwa na dosari lakini Ngei alisema Muhoro ambaye alikuwa mkubwa wake, ndiye alizima stima na kuwakisha tena ndipo ukalipuka katika duka hilo.

Pia Muhoro alisema kwamba jenereta ya Nakumatt ilikuwa na dosari lakini wachunguzi waliofika siku tatu baada ya moto kuteketeza duka hilo waliipata ikiwa katika hali nzuri.

“Baada ya kutathmini ushahidi uliowasilishwa mbele yangu, ni wazi KPLC inafaa kulaumiwa kwa mkasa huo,” Jaji Mong’are alisema akitoa uamuzi.

Baada ya kufikia uamuzi huo, Jaji huyo aliiamuru KPLC ilfidie Woolworths zaidi ya Sh500 milioni kama fidia.

Pia Jaji Mong’are aliamuru KPLC ilipe Woolworths kodi ya nyumba Dola za Marekani-USD- 3,085,600 (Sh416,556,000).

Mahakama iliamuru KPLC iilipe Sh7.4 milioni ada za ardhi na Sh58.5 milioni thamani ya nyumba kuanzia Februari 2009.

Jaji Mong’are aliagiza KPLC pia ilipe faida ya pesa hizo zaidi ya Sh500 milioni.