Kenya ni namba moja kwa wanaume watanashati zaidi Afrika, utafiti wasema
NA LABAAN SHABAAN
KENYA imeorodheshwa kuwa namba moja kwa wanaume ‘warembo’ sana barani Afrika.
Haya ni kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na jarida la Insider Monkey.
Hii ni tovuti ya kibiashara ambayo hufuatilia masuala ya fedha na uwekezaji.
Kulingana na utafiti huu, wanaume wa Kiafrika wanaaminiwa kuwa wanapendeza sana ikilinganishwa na wale wa Ulaya na Asia.
Kenya ikiwa juu ya jedwali la wanaume watanashati Afrika, wale wa Nigeria na Ethiopia walichukua nambari mbili na tatu mtawalia.
Wanaume wa Rwanda, Afrika Kusini na Angola waliibuka nambari nne, tano, na sita kwa usanjari huo.
Mwanamitindo wa Kenya ambaye ni maarufu duniani Kevin Oduor ndiye mwanamume anayetamaniwa zaidi.
Bw Oduor, anayeamini pia wanaume ni warembo na wana azma, amechangia kwa Kenya kuorodheshwa bora.
Lakini baadhi ya Wakenya mitandaoni hawaamini kama ripoti hii ni sahihi.
“Kulikuwa na matatizo ya kimitambo wakati wa utafiti huu,” aliandika Mkenya mmoja.
Mwingine akasema: “Kumbe ndiyo maana niliambiwa nikae nyumbani utafiti ukifanywa?”
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, Tanzania iliibuka nambari 11 huku Uganda ikiwa nambari 10.
Uchunguzi huu uliangazia mataifa 20 Afrika ambapo Senegal, Zimbabwe, na Cameroon walishika nafasi za 18, 19 na 20 mtawalia.