Wilson Lemkut: Shujaa aliyewaokoa watoto 16 ziwani Baringo
HII ni simulizi iliyojaa ushujaa. Simulizi ya Bw Wilson Lemkut aliyewaokoa watoto 16 waliokuwa karibu wafe maji katika mkasa wa boti katika Ziwa Baringo.
Tukio hili la ujasiri lilileta afueni kiasi katika kipindi ambapo familia zilizowapoteza wapendwa wao wakati wa mkasa huo, zingali zinaomboleza.
Watu saba waliaga dunia lakini ukakamavu wa Bw Lemkut ambaye ni baba wa watoto 12 na mkazi wa kisiwa cha Kokwa, ulisaidia hadi wengi wakaponea kifo.
“Mtoto wangu alikuja nyumbani na kuniambia kuna boti imezama na ina watu. Hapo ndipo nilitoka nyumbani kuenda kuwaokoa,” alisema Bw Lemkut.
Baada ya kutambua hatari iliyokuwepo, Bw Lemkut bila kupoteza muda aliamua kukabaliana na mawimbi hatari ya maji.
Yeye, pamoja na wana wake wawili, waliposikia kilio cha vijana hao waliokuwa kwa boti ya kutoka Salabani, walianza uokozi mara moja.
Ndani ya robo saa, walifika katika eneo la ajali ambapo waliwakuta watoto hao wakitapatapa majini huku wakishikilia boti na tanki ya mafuta.
Hapa, ‘masaa yalikuwa ni mchache na mambo hayakuwa mengi.’ Wajibu ulikuwa mmoja tu – uokozi ndani ya nukta chache.
Licha ya uzani wa boti kuongezeka na mawimbi makali kuvuma, Lemkut aliendelea kujitahidi bila kufa moyo kuokoa mioyo mingine.
“Tulipofika eneo la ajali wote waliomba Mungu watoshee boti yetu. Walikuwa wanatetemeka. Ni vizuri kwa sababu walikuwa vijana na si wazee,” alisema Bw Lemkut.
Kwa hakika, ilimchukua robo saa kutoka kisiwani na kufika eneo la mkasa.
Na ikamgharimu nusu saa kuwakomboa wote na kuwarejesha ufuoni.
Lakini sekunde chache baadaye, tukio la kuatua moyo lilitokea. Mvulana mwenye umri wa miaka 17 alikata roho pindi tu alipofika ufukweni.
“Kuna mmoja tuliokoa ambaye karibu aachilie boti iliyopinduka ila alifariki baadaye,” alisikitika Bw Lemkut.
Lemkut alisimama kidete alipohitajika licha ya kukumbana na hali hatari.
Tukio hili linachora taswira ya watu wa kawaida wanaoibuka katika matukio yasiyo ya kawaida na kuwa mashujaa.