Habari za Kitaifa

Familia ya Moi yachangisha pesa za matibabu ya mjukuu

April 26th, 2024 2 min read

JOSEPH OPENDA Na KENNEDY KIMANTHI

JAPO aliyekuwa Rais wa Pili wa Kenya, Hayati Daniel Moi alikuwa kiongozi wa kuheshimika Afrika na mmoja wa watu matajiri zaidi nchini, miaka minne baada ya kifo chake, familia yake imeshindwa kumudu gharama ya vitu vya kimsingi kama huduma ya afya.

Kesi ya urithi inayoendelea mahakamani imezuia matumizi ya mamilioni ya pesa aliyoacha kwenye benki.

Pesa hizo zikishikiliwa katika benki mbalimbali nchini, jamaa za Moi wanapitia wakati mgumu kujikimu kimaisha.

Hali ya familia pana ya Moi ilijitokeza Jumatano jijini Nakuru wakati wa hafla ya kuchanga fedha za kumsaidia mjukuu wa Rais huyo wa Pili wa Kenya, mwenye umri wa miaka 14, ili apewe huduma za matibabu Nairobi.

Harambee hiyo iliongozwa na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, mmoja wa wandani wa karibu wa Rais wa sasa William Ruto.

Hatua hiyo imefasiriwa kama sehemu ya mpango wa kuyeyusha ushawishi wa kisiasa wa familia ya Moi katika eneo la Rift Valley ambako Rais Ruto anatoka.

Lakini kimsingi, harambee hiyo ilifichua kuwa mali ya Mzee Moi iko katika hatari ya kumalizika.

Mtoto huyo ni mwanawe marehemu Jonathan Toroitich, ambaye ni kifungua mimba wa Mzee Moi.

Mvulana huyo amekuwa akiugua aina fulani ya saratani lakini hangeweza kupokea matibabu kutokana na changamoto za kifedha.

Mjane wa Jonathan na mamake mtoto huyo, Bi Faith Nyambura Moi, awali alikuwa ameomba msaada kutoka kwa wahisani ili aweze kugharimia matibabu ya mwanawe.

Kufuatia ombi hilo, viongozi wa Rift Valley walijitokeza na kufaulu kuchanga jumla ya Sh6,150,000 za kugharimia bili ya matibabu.

“Sasa tunataka ujiandae kwa safari ya kuelekea India ili mtoto aanze kupokea matibabu. Ni heri tuambiwe kuna uhaba wa fedha baada ya matibabu kuanza badala ya wakati huu ambapo matibabu hayajaanza. Huyu ni mtoto mdogo ambaye anastahili kusaidiwa na jamii,” Bw Sudi akasema.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ya kuchanga pesa ni pamoja na Mbunge wa Mogotio Reuben Kiborek, aliyekuwa Mbunge wa Soi Caleb Kositany na Waziri wa Vyama vya Ushirika Simon Chelugui.

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii, walituma michango yao.