MWANAMIPASHO: Sina chuki, ila hapa kwa TID mwanishangaza
NA MWANAMIPASHO
ILA Wakenya huwa mnanishangaza sana.
Yaani mtu akitrendi tu kwa vitu vya kipuzi, hao sisi tushaanza kuwashobokea kuwapa dili na muda wetu wakati hawazistahili.
Juzi tu huyu mwanamuziki Mzee TID, ametrendi kwa zile sehemu, sehemu za video zake akiwakebehi watu kwa lugha ya kizungu.
Sasa ghafla mlishafikia kumpa shoo Nairobi. Yaani nini sasa kwa kweli? Maana sielewi na siwaelewi?
Msela licha ya mbwembwe zake kule kwao Tanzania na kukesha akiruka kama panzi kutoka kituo kimoja cha radio hadi kingine akifanya mahojiano huku akiwakemea wasanii wenzake kwamba hawajui kuimba, bado tu hajafanikiwa kupewa shoo.
Huku Kenya kwa bahati nzuri au mbaya, msela katrendi kwa sehemu ya video fulani akiongea kizungu fulani hivi na ghafla mnamwitia shoo.
Miaka yote hiyo kaka mkubwa shoo hazioni kwao leo mnampatia shoo kiulaini kisa kutrendi kwa ushuzi wake?
Mwanzo kabla mseme nina chuki, naomba tuwekane sawa. TID ni msanii mzuri, mimi binafsi nimelelewa na kukua nikimsikiza huyu msela kipindi akiwa kwenye ubora wake, akiwa Top In Dar kikweli.
Nakuaminia TID kila alipokuwa akiingia studio alikuwa akiachia mawe ya kukuumiza.
Nakumbuka lile jiwe la Aisha alilotutupia miaka hiyo, kipindi najifunza kupenda hawa mademu. Aisee! jiwe liliniingia hadi kwenye maini.
Huyo ndiye TID ninayemkumbuka mimi, sio huyu wa sasa anayeng’ang’ana sana kuzungumziwa, akijisifia wakati hakuna nyimbo anazotoa.
Sasa hiyo shoo mumempa hivi mumempa kwa sababu ana nyimbo kadhaa mpya au? Maana ninavyoufuatilia muziki wa bongo flava, lazima ningekuwa nimepata kusikia ngoma hata moja.
Hii kasumba yetu ya kupenda kufagilia upuzi hunichosha sana kwa kweli. Jalangó alishawahi kusema Wakenya tuna kasumba ya kuja pamoja kufurahia na kusherehekea jambo la kipuzi upuzi upepo huo ukipita tunasonga kwa tukio jingine.
Sisemi msimpe TID shoo lakini ninachouliza Sheikh, je huyo jomba anastahili kupewa shoo sasa hivi wakati hatuoni akifanya lolote la muhimu kwenye muziki wake?
Kwao hajapata kitu, sisi ndio tunampa. Kwa nini tunapenda kusherehekea upuzi wanangu? Na ndio maana siku zote tasnia yetu ya burudani haitawahi kusonga wakati Watanzania wao wakiendelea kupanda.
Mumeona tayari wameshafikia levo ya kufanya kazi na mashirika makubwa kama BET na MTVBas. Hilo mumeliona sio? Mwaona tutafika huko lini kama tukiendelea kusherehekea upuzi?