Liverpool kwenye mizani ya West Ham United
NA MASHIRIKA
LONDON, UINGEREZA
LIVERPOOL watasonga hadi nafasi ya pili kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa saa kadha iwapo wataruka kamba ya wenyeji West Ham United katika uwanja wa London Stadium, Jumamosi alasiri.
Nao Manchester United watakuwa nyumbani dhidi ya Burnley baadaye Jumamosi jioni kutafuta ushindi utakaoimarisha matumaini yao ya kumaliza sita-bora ili kufuzu kwa kombe la Europa League msimu ujao.
Vile vile, nambari 18 Luton Town, Burnley (19) na wavuta-mkia Sheffield United pia zitakuwa zikinogesha kukurukakara za kuzinasua kutoka eneo hatari la kushushwa ngazi.
Lakini mechi kati ya West Ham United na Liverpool ndio inayotarajiwa kuvutia mashabiki wengi ikizingatiwa kwamba West Ham walio katika nafasi ya nane watakuwa wakipigania ushindi baada ya kusuasua mfululizo katika mechi zao zilizopita dhidi ya Fulham na Crystal Palace. Walishindwa kwa 2-0 na 5-2 katika mechi hizo mbili.
Ushindi kwa wenyeji vile vile utawafanya West Ham kujiongezea matumaini ya kumaliza ligi hiyo miongoni mwa saba bora na kufuzu kwa michuano ya bara Ulaya, msimu ujao.
Kichapo kitakuwa hasara kwa kikosi hicho cha kocha David Moyes ambacho kimebakisha mechi nne kutamatisha msimu huu wa 2013/2024.
Liverpool wanaingia uwanja baada ya hapo awali kushindwa mara mbili mfululizo, juzi na Everton iliyowachapa 2-0, matokeo ambayo yamepunguza matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa msimu huu, ambao pia unanganganiwa na Arsenal na Manchester City.
Vijana hao wa kocha Jurgen Klopp wanakamata nafasi ya tatu nyuma nyuma ya Manceschester City na vinara The Gunners kwa pengo la pointi tatu. Habari za hivi punde zimesema kwamba tayari tiketi za mashabiki kuingia uwanjani humo zimeisha.
Klopp amesema hajapoteza matumaini huku akikisitiza kwamba yaliyowapata yanaweza pia kuangukia Arsenal na Manchester katika mechi zilizobakia.
West Ham wameshinda mechi moja tu kati ya saba zilizopita, huku kichapo cha 5-2 kutoka kwa Crystal Palace kimiwaacha katika nafasi ya nane jedwalini.
Historia yao dhidi ya Liverpool ni nzuri lakini haitakuwa kazi rahisi mbele ya kikosi cha Klopp ambaye hajawahi kuandikisha ushindi mara tatu katika msimu mmoja, ingawa wanajivunia ushindi mara 12 dhidi ya 14 ligini.
Nyota wao Jarrod Bowen anatarajiwa kurejea, wakati Klopp akiendelea kuunda kikosi bila mastaa kadhaa wakiwemo Diogo Jota, Thiago Alcantara na Joel Matip.
West Ham maarufu kama The Hammers watajaribu wawezavyo kuzuia kichapo cha tatu mfululizo, hasa dhidi ya Liverpool ambao kiwango chao kimeshuka.
Ratiba ya Jumamosi:
West Ham United vs Liverpool (2:30pm), Wolves vs Luton Town (5pm), Fulham vs Crystal Palace (5pm), Newcastle United vs Burnley (5pm), Manchester United vs Sheffield United (5pm), Manchester United vs Brentford (7:20).
Jumapili:
Tottenham Hostpur v Arsenal (4pm), Nottingham Forest v Manchester City (6:30).