Watu saba waokolewa baada ya lori lao kusombwa na mafuriko
NA MWANDISHI WETU
WATU saba wameokolewa kutoka kwa Mto Kwa Muswii na kupelekwa katika hospitali ya Sultan Hamud, Shirika la Msalaba Mwekundu nchini, Kenya Red Cross, limesema Ijumaa.
Limeongeza kwamba shughuli ya uokoaji inaendelea.
Inakadiriwa watu 10 walitumbukia majini baada ya lori kusombwa na mafuriko wakijaribu kuvuka Mto Muswii katika Kaunti ya Makueni.
Katika mojawapo ya video ambayo imenaswa na walioshuhudia, watu waliokuwa kwenye lori hilo walianza kutapatapa kwa kujaribu kuogelea huku maji yaliyokuwa yanaenda kwa kasi yakiwalemea.
Waliokuwa wanatazama walianza kupiga mayowe.
Kabla ya Red Cross, hakukuonekana waliojaribu kuwaokoa kwa hofu ya kusombwa pia, wengi wao wakiwaambia kushikilia mti au chochote kinachoweza kushikilika.
Usafiri katika barabara ua Kasikeu-Sultan Hamud umekatizwa baada ya mto huo ambao unaanzia katika kaunti jirani ya Kajiado kuvunja kingo zake.