Habari za Kitaifa

Ndani ya ziara ya Ruto nchini Tanzania, akutana na mvua huko

April 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WANGARI

RAIS William Ruto mnamo Ijumaa aliungana na Rais wa Tanzania Samia Suluhu kusherehekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa iliyokuwa Tanganyika na visiwa vya Zanzibar huku ziara yake nchini humo ikiibua hisia mseto miongoni mwa Wakenya.

Rais Ruto aliondoka Alhamisi usiku kujumuika na Watanzania katika sherehe hizo kabla ya kusafiri nchini Zimbabwe kwa ziara ya siku mbili ambapo amealikwa kama mgeni wa heshima katika awamu ya 64 ya Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara Zimbabwe, jijini Bulawayo.

Taarifa ya Ikulu ilitaja ziara ya Rais Ruto nchini Tanzania kama “ishara ya uhusiano wa dhati, ujirani mwema na ushirikiano imara na Jamhuri ya Tanzania na raia wake”.

Huko Dkt Ruto na mwenyeji wake walivumilia mvua na kijibaridi.

Dkt Ruto alionekana akiwa na mwavuli pamoja na Mama wa Taifa Rachel Ruto wakiingia uwanjani.

Dkt Suluhu naye alionekana akiwa amevalia kabuti nzito kujikinga dhidi ya kijibaridi kikali.

Sherehe zimeandaliwa katika uwanja wa kitaifa wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Wamekuwepo pia marais Sheikh Mohamud (Somalia), Evariste Ndayishimiye (Burundi), Azali Assoumani (visiwa vya Comoros) na Hussein Ali Mwinyi (Zanzibar).

Hata hivyo, baadhi ya Wakenya wamechukulia ziara hiyo ya Dkt Ruto kama kinaya hasa ikizingatiwa kuwa marais wa mataifa jirani, katika siku za hivi karibuni, wameonekana kujiepusha kuhudhuria matukio muhimu nchini Kenya.

Katika maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri, mwaka 2023, marais Suluhu (Tanzania), Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda) na Evariste Ndayishimiye (Burundi) hawakujitokeza.

Ni Rais Hussein Mwinyi (Zanzibar) na Sahle-Work Zewde (Ethiopia) pekee walioitikia mwaliko wa sikukuu hiyo muhimu katika historia ya Kenya, jambo ambalo si la kawaida kwa mataifa jirani katika jumuiya ya Afrika Mashariki, na lililoibua maswali tele kuhusu uhusiano wa mataifa haya jirani.

Rais Mwinyi aliyemwakilisha Bi Suluhu alisema rais huyo alikosa kuhudhuria kutokana na mafuriko yaliyokumba Tanzania Kaskazini huku Naibu Waziri Mkuu wa Uganda, Rebecca Kadaga, aliyehudhuria kwa niaba ya Bw Museveni akisema tu “Rais “hakuweza kuhudhuria”.

Ziara ya Rais Ruto imejiri wakati ambapo taifa hili linakabiliana na mafuriko na maporomoko ya ardhi kutokana na mvua ya masika inayoendelea kunyesha nchini huku watu kadhaa wakiangamia, kuachwa bila makao na kukadiria hasara kubwa.

Tukio hilo la marais wa mataifa jirani kususia mwaliko wa Kenya na hatua zao zilizofuatia, zimeonekana kutia doa uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa ya Afrika Mashariki.

Rais Ruto, hata hivyo, alipuuzilia mbali madai hayo akisema mahusiano baina ya Kenya, Tanzania na Uganda ni “imara” na hali kwamba hawakuhudhuria sherehe za Sikukuu ya Jamhuri sio ishara kuwa uhusiano baina yao umezorota.

“Huwa ninahudhuria sikukuu za kitaifa za mataifa mengine? La. Hilo linamaanisha kuna tatizo? La,” alisema Dkt Ruto akijibu maswali ya wanahabari walioalikwa katika Ikulu ya Nairobi mnamo Desemba 2023 kudadisi masuala mbalimbali yenye umuhimu wa kitaifa.

Maelezo zaidi na Hassan Wanzala