Viongozi wanawake Murang’a vitani kisiasa, kulikoni?
NA MWANGI MUIRURI
KAUNTI ya Murang’a katika siku za hivi karibuni imeibuka kuwa ya miereka ya kisiasa huku baadhi ya wanasiasa wake wakirushiana cheche mitandaoni na katika mikutano ya hadhara.
Viongozi wa kike nao hawajaachwa nyuma ambapo kila kuchao wanaonekana wakilumbana kwa mitandao, hadharani na pia kimasomaso huku wakirushiana cheche za maneno na matusi motomoto.
Mnamo Aprili 15, 2024, katika uwanja wa Shule ya Upili ya Kigumo Bendera, wenyeji walishuhudia miereka ya wafuasi wa baadhi ya viongozi wa kike wakitandikana ngumi na mateke.
Nao viongozi hao walikuwa kwa nusu saa wakitusiana kwa maneno machafu tusioweza kuchapisha.
Wafuasi wa Waziri wa Ardhi Alice Wahome, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Betty Maina, Mbunge wa Maragua Mary wa Maua, wale wa mbunge maalum Sabina Chege na wale wa Seneta maalum Veronica Maina walikabiliana kwa ghasia tosha.
Hata walinzi wa viongozi hao walianzana kutwangana wapenda amani nao wakionekana kuhangaika kudhibiti hali.
Vita hivyo vilitokea katika hafla ambapo Bi Maina alikuwa ameiandaa kupiga jeki wasukaji wa vyondo–aina ya vikapu–vya kitamaduni.
Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa na mwenzake wa Vyama vya Ushirika Simon Chelugui ndio walikuwa wageni wa heshima na walionekana wakikingwa na maafisa wa polisi wasiathirike katika fujo hizo.
Kwa mujibu wa mdadisi wa siasa za eneo la Mlima Kenya Prof Ngugi Njoroge, vita hivyo vya kisiasa katika Kaunti ya Murang’a vinachochewa na baadhi ya misukumo, mmojawapo ukiwa ni ule wa kusaka ubabe ukihusisha wafuasi wa Naibu Rais Rigathi Gachagua na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.
“Huo ndio uhasama mkuu ulio na wanasiasa wa Murang’a na ambapo licha ya Bw Nyoro na Bw Gachagua kusema hadharani kwamba hawana vita, nyanjani ni wazi kwamba kuna mawimbi ya upinzani wao ambayo yanaendelea kuvuma,” akasema Prof Njoroge.
Ndani ya mrengo wa Bw Gachagua pia kumesemwa kuwa na vita vya wanasiasa walio na utiifu kwake wakibishania ni nani anafaa kupokezwa rasilimali za kufadhili miradi ya kusaka ushindi katika miereka hiyo ya ubabe.
“Shida nyingine tuliyo nayo hapa Murang’a ni kuhusu nafasi ya chama cha Jubilee katika siasa za serikali kwa kuwa baada ya kuamua kushirikiana na Bw Gachagua na kumtambua kama kinara wa siasa za Mlima Kenya, kuna manufaa ambayo yanakiendea chama hicho na ambayo yalifaa kuwa ya wafuasi wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA),” asema aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi.
Aliongeza kwamba ni katika vita hivyo vya kudhibiti manufaa ambapo wanasiasa wa UDA wanaojipata wakisukumwa nje ya ushawishi, wanazindua misururu ya vita na wafuasi wa Jubilee wanaowasukuma nje.
Ndani ya vita hivyo pia kunasemwa kuwa na uchochezi wa baadhi wa maafisa wa usalama ambao katika harakati zao za kikazi, wamekwaruzana na baadhi ya wanasiasa.
“Maafisa hao wa usalama wameonekana kuwapa usaidizi wapinzani wa wanasiasa ambao hupigana na maafisa hao kutandaza vita vya kisasi,” akasema mmoja wa wanasiasa wa Kaunti hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mwanasiasa huyo alifichua kuhusu mkutano wa afisa mmoja wa ngazi ya juu katika usalama wa kaunti pamoja na mwanasiasa mmoja mbishi katika Mkahawa wa Nokrass “na ndipo baada ya wiki moja vile vita ya Kigumo vya Aprili 15, 2024, vikazuka vikiongozwa na mwanasiasa huyo huku maafisa wa usalama wakionekana kuwa mashahidi tu bila kufanya lolote”.
Masafisa hao wa usalama pia wamesemwa kusombwa na siasa za kitaifa ambapo “tuko na ukoloni wa maafisa wengi wa usalama hapa Murang’a kuwa wa kabila moja ambalo pia liko katika vita vya ubabe wa Mlima Kenya katika uchaguzi wa 2027”.
Masuala mengine ambayo yametajwa kuwa ya kuchangia ghasia za kisiasa katika kaunti ya Murang’a ni pamoja na hofu ya uchaguzi wa chama cha UDA.
Pia, kuna cheche kwamba kuna uwezekano wa mmoja wa wanasiasa wakuu nchini kufadhili siasa za mgawanyiko ili kudhibiti eneo hilo na pia “tabia mbaya za kawaida za wanasiasa” vikichangia pia ghasia.