Lugha, Fasihi na Elimu

Changamoto tele shule zikitarajiwa kufunguliwa

April 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WINNIE ATIENO

SHULE zitafunguliwa rasmi kuanzia Jumatatu kwa muhula wa pili huku taasisi za masomo zikikumbwa na changamoto kadhaa.

Changamoto hizo zinajumuisha janga la mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa katika kaunti mbalimbali nchini, serikali kuchelewa kutoa fedha kwa taasisi za masomo na ukosefu wa miundombinu.

Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari nchini, (Kessha), Jumamosi kilisema kwamba walimu wakuu wanapitia changamoto hasa pale ambapo serikali inakosa kutuma pesa kwa wakati.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama hicho, Bw Willy Kuria ana matumaini kuwa serikali itatuma fedha hizo shule zitakapofunguliwa.

Akizungumza na Taifa Jumapili jijini Mombasa wakati wa mkutano na walimu wakuu wa shule za kitaifa, Bw Kuria alisema muhula wa pili huwa na shughuli nyingi.

Bw Kuria alisema muhula wa pili ambao ni mrefu zaidi ikilinganishwa na mihula mingine ni muhimu kwani wanafunzi wa kidato cha nne hujiandaa kwa muhula wao wa tatu kufanya mtihani wao wa mwisho.

“Pia tutakuwa na kongamano letu la kila mwaka la Kessha hapa Mombasa kwa hivyo ni muda wenye shughuli nyingi,” aliongeza.

Wakati wa kongamano lao la Kessha, wakuu wa shule walikutana Mombasa kujadili masuala yanayoathiri shule za upili za umma nchini na kutoa mapendekezo kadhaa.

Bw Kuria alisema hatua ya wizara ya elimu ya kuchelewa kutoa fedha ni changamoto kubwa hasa katika uendeshaji wa shughuli za shule. Alisema shule zilipata fedha mnamo Aprili 26, 2024.

Serikali ilitoa Sh30.5 bilioni kugharamia elimu ya sekondari, mikopo na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu. PICHA | MAKTABA

Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu, alisema Sh7 bilioni zitatumika kuwafadhili wanafunzi wa shule za umma katika sekondari za daraja la chini huku Sh16 bilioni zikiwagharamia wanafunzi chini ya mpango wa elimu ya bure.

“Tumeamua kutoa kidogo tulichonacho. Kwa sasa, wizara haina fedha,” waziri Machogu alisema.

Hata hivyo, Bw Kuria alisema fedha hizo hazitoshi.

Kwa upande mwingine, alisema kwamba shule zinazoathirika zaidi pesa zikichele ani zile za kutwa.

Hii ni kwa sababu baadhi ya wazazi huchelewa kulipa karo.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA), Silas Obuhatsa, alizitaka bodi za usimamizi wa shule kuzuru shule zao kabla zifunguliwe ili kuhakikisha kwamba ziko salama kwa wanafunzi hasa katika maeneo kama Budalang’i na Tana River.

“Hii itasaidia pakubwa ili tuweze kujua ikiwa shule hizo ni salama kwa wanafunzi,” akasema Bw Obuhatsa.

Haya yanajiri huku maeneo kadhaa nchini yakikumbwa na mafuriko.

Baadhi ya shule zimefunikwa na mafuriko jambo ambalo huenda likaathiri masomo kwa muda.