Farasi ni wawili sasa EPL ‘Ndovu’ Arsenal wakihitajika kukomoa Spurs kwa vyovyote vile
NA TOTO AREGE
KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta amewaomba vijana wake kuweka ushindani wao wa kaskazini mwa London kando, wanapojiandaa kukabiliana na mahasimu wao wa jadi Tottenham Hotspur katika debi ya London kuanzia saa kumi alasiri Jumapili.
Ajabu ni kwamba Arsenal, wamecheza mechi nne tangu Tottenham walipocheza mara ya mwisho – wakipoteza kwa Aston Villa ligini na Bayern Munich katika robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya lakini wakawashinda Wolves na Chelsea kusalia kileleni.
“Tumecheza katika Uwanja wa Tottenham Hotspur mara chache na naweza kusema kwa hakika ni sehemu nzuri ya kuchezea. Lazima tuweke ubishi kando na tunatakiwa kujitolea katika mechi hiyo kwa sababu tunafahamu ina umuhimu gani kwetu,” alisema Arteta.
The Gunners wanajua watasalia kileleni wakiwa na ushindi ili kusonga hatua ya kukaribia taji la kwanza la EPL katika miongo miwili, wakati Arsenal ya Arsene Wenger ilipotwaa taji huko White Hart Lane mnamo 2004.
Mwenzake wa Tottenham Ange Postecoglou naye amewataka vijana wake kuzidisha makali yao ya ushambuliaji licha ya kukabiliana na timu yenye rekodi bora ya ulinzi katika ligi msimu huu.
Katika mechi nyingine baadaye leo, mabingwa watetezi Manchester City, wataendelea na jitihada za kubeba ubingwa wa nne mfululizo ugenini dhidi ya Nottingham Forest inayopambana kusalia EPL msimu ujao.
City wataingia mchezoni baada ya ushindi mnono wa 4-0 dhidi ya Brighton Alhamisi iliyopita bila huduma za mshambuliaji tegemeo Erling Haaland.
Sasa wako pointi moja nyuma ya The Gunners wakiwa na mchezo mkononi. Ikiwa watapata ushindi dhidi ya Nottingham watapanda hadi kileleni mwa jedwali.
Forest walitoka sare ya 1-1 dhidi ya City msimu uliopita lakini kwa hakika hawana kiasi cha kutosha kusimamisha timu ya Guardiola katika fomu ya aina hii.