Akili Mali

Biashara ya juisi ya mua ni mgodi wa pesa, faida za kiafya

April 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LABAAN SHABAAN

JUISI ya miwa haipendelewi sana na watu ukilinganisha na maji ya matunda hasaa nyakati za joto lakini biashara zinazouza sharubati hii zimeongezeka.

Kulingana na wataalamu wa afya, mbali na kukabili athari ya jua kali kukamua maji mwilini, sharubati ya miwa ina virutubisho muhimu vya kudumisha afya bora.

Miongoni mwa manufaa mengine, kinywaji hiki huhakikisha mwili una maji, viwango vya juu vya nguvu, kusaidia usagaji chakula tumboni, na kudumisha afya ya ini.

Mfanyabiashara Joshua Muwa amekuwa mchuuzi wa juisi ya miwa kwa zaidi ya miaka 10 ambaye ameona kuna haja ya kupanua wigo wake wa biashara.

Mseto wa maji ya miwa, tangawizi, na ndimu umevutia wateja wengi katika biashara yake eneo la Ruaka, Kaunti ya Kiambu.

Biashara hii hupata faida kubwa sana wakati wa maonyesho ya kilimo.

Kwa hivyo, msakatonge huyu huwa ange sana kujua kalenda ya maonyesho ya kilimo nchini.

Mfanyabiashara wa juisi ya mua, Bw Joshua Muwa akata mua kabla ya kuchakata kwa mashine kuunda juisi. PICHA | LABAAN SHABAAN

Aghalabu watu wengi hukongamana katika maonyesho ya kilimo kujifahamisha masuala mbalimbali ya zaraa.

Bw Muwa huwa tayari kuyahudhuria ili kufaidika na mahudhurio makubwa ambayo hushuhudiwa.

Kuuza maji ya miwa hakukuwa azma yake kwanza ila alikukumbatia baada ya kuanza kuuza vyombo vya jikoni.

“Tumekuwa katika maonyesho ya kilimo kwa miaka. Kuna kipindi tuliona upenyu watu wakitaka kukata kiu na kuwa na nguvu sababu ya kutembea sana,” anasema Bw Muwa.

“Hapo ndipo tulianza kuuza sharubati hii kwa waliohudhuria shoo za kilimo.”

Yeye huuza juisi hii kwa angalau Sh50 kwa glasi ndogo na kopo kubwa huuzwa Sh100.

“Wateja wengine hupendelea kuwa na viungo kwa viwango tofauti. Kwa mfano, kuna wateja wanataka tangawizi nyingi zaidi ya ndimu. Hapo mimi huwahudumia wanavyotaka lakini bei haibadiliki,” anaeleza.

“Kwamba nimefanya biashara hii kwa miaka ina maana ninaifurahia. Kama ningekuwa sifanyi vizuri, ningefunga biashara hii,” anaongeza bila kufichua masuala yake ya fedha.

Mjasiriamali huyu anaambia Akilimali kuwa ameng’amua kuhusu utamu wa miwa kutoka ukanda wa Nyanza hasa maeneo ya Kisii.

“Tunapendelea miwa ya Kisii kwa sababu ni mitamu sana na pia bei yake ni afadhali. Kwa kawaida, sisi hununua kwa wingi na kuhifadhi kwenye stoo,” anaeleza.

Kampuni yake ya Kitchen Solutions hufunza wanabiashara wengine jinsi ya kuandaa juisi hii.

Wao hutumia fursa hii pia kuwauzia mitambo ya kuchakata miwa ambayo huuzwa kwa angalau Sh65,000.

Mtambo wa kutumika wakati wa utengenezaji wa juisi ya mua. Mashine ndogo huuzwa kwa Sh65,000. PICHA | LABAAN SHABAAN

Bw Muwa ana ndoto ya kufungua matawi mengine katika sehemu tofauti nchini baada ya kuona kuwa ni biashara yenye uwezo wa kupata wateja wengi.