Habari za Kitaifa

Machogu atetea kutuma agizo la kusitisha ufunguzi wa shule usiku wa manane

April 29th, 2024 2 min read

DAVID MUCHUNGUH NA LABAAN SHABAAN

WAZIRI wa Elimu Ezekiel Machogu ametetea tukio la kutuma taarifa ya kusitisha ufunguzi wa shule usiku wa manane kwa wiki moja.

Hii ni baada ya kupokea shutuma kali kutoka kwa wananchi kutoka pembe zote za taifa akikemewa kwa kuchelewa kutoa taarifa hiyo.

Kupitia mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Machogu alisema wizara yake ilichukua hatua hiyo ili kuokoa maisha ya wanafunzi.

Bw Machogu alisema kuwa wizara yake imepokea takwimu kuonyesha kuwa miundomsingi ya usafiri imeharibiwa vibaya na mafuriko yanayoendelea kuponda nchi.

Kwa mujibu wa waziri, miundombinu ya shule mbalimbali pia iliharibiwa. Haya ni kulingana na takwimu zilizokusanywa Jumamosi na Jumapili ambazo zilisaidia serikali kuchukua hatua hiyo.

“Tunaongea kuhusu maisha ambayo ni ya muhimu sana achia mbali masumbufu (ya tangazo la kuahirisha tarehe ya ufunguzi) ambayo watu wanaongea kuhusu.

 Kama shule zingefunguliwa katika hali hii na jambo baya lifanyike, wangenilaumu. Nimechagua kuokoa maisha. Tunatathmini hali kwa karibu sana,” aliambia Taifa Leo.

Juma lililopita Katibu wa Wizara ya Elimu Prof Belio Kipsang alitangaza kuwa shule zingefunguliwa mvua ikiendelea, isipokuwa shule ambazo zimeathiriwa na mafuriko.

Lakini wazazi waliamkia taarifa ya kushtusha baada ya serikali kuahirisha siku ya ufunguzi.

Shule nyingi za umma zilikuwa zimeratibiwa kufunguliwa leo. Baadhi ya wazazi waliowatuma watoto shuleni walibidika kurudi kuwachukua na kulaumu serikali kwa kutowaarifu mapema.

“Si sawa! Kutoa taarifa kwa wakati sahihi ni muhimu sana kwa shirika lolote hususan kuhusiana na elimu ambapo kila mtu anahusika. Hebu fikiria wazazi wengi walikuwa wamekatia wanafunzi tiketi ya treni ya SGR kitambo na tayari walianza safari kisha wakaarifiwa ufunguzi umeahirishwa,” mzazi mmoja alilalamika.

Bw Machogu alisema kuwa walichunguza data kutoka kwa wakurugenzi wa kaunti wikendi kisha wakashauriana na idara ya hali ya anga.

Waziri alijitetea kuwa ripoti walizopokea ziliwezesha serikali kutangaza kuahirishwa kwa tarehe ya ufunguzi.

Juma lililopita wizara hii ilielekeza maafisa wake wa nyanjani kukusanya takwimu kutoka taasisi zote za elimu ya msingi ili kutathmini utayari wa shule kwa masomo ya muhula wa pili yaliyoratibiwa kuanza Jumatatu Aprili 30, 2024.

Bw Machogu alisema ilikuwa vigumu kukusanya data kwa sababu  walimu wakuu wamekuwa katika likizo.

“Kama kuna wanafunzi shuleni sasa, wanaweza kubaki huko ili wasijiweke katika hatari wanaporudi nyumbani. Tunabuni vikosi vya kaunti ili vitupe maelezo zaidi kuhusu hali ilivyo,” waziri alisema.

Bw Machogu pia alisema nyingi ya shule za kibinafsi ziliratibiwa kufunguliwa Jumanne wala si Jumatatu.

“Madarasa yako sawa katika shule nyingi lakini misala imeathiriwa. Vyoo haviwezi kutumika kwa sababu vimejaa maji na vingine vimezama kwa hivyo ni hatari kwa afya,” waziri alidokeza.