Ni rasmi sasa, farasi ni wawili EPL baada ya Liverpool kugeuka punda
KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, amekiri kuwa lazima washinde mechi zao zote ili kupiku Arsenal katika vita vya kunyanyua Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.
Guardiola ameonya masogora wake kwamba hawawezi dondosha hata alama moja katika nafasi ya pili kwenye pilkapilka za kutetea taji lao na pia kuweka historia kama timu pekee iliyozoa EPL misimu minne mfululizo.
Mkufunzi huyo raia wa Uhispania alisema anatarajia Arsenal kushinda mechi zao zote zilizosalia baada ya vinara hao kuzamisha majirani Tottenham Hotspur 3-2 mnamo Jumapili.
“Tungependa sana washindwe, lakini hatuwezi kuamua watakachofanya,” Guardiola alitanguliza baada ya vigogo wake kulemea Nottingham Forest 2-0 katika uwanja wa City Ground mnamo Jumapili usiku kupitia mabao ya Josko Gvardiol na Erling Haaland.
“Kuna mechi nne zimesalia (kwetu). Sidhani wao watatupa pointi zozote, kwa hivyo tunajua fika matokeo tunayofaa kupata,” akaongeza Jumapili usiku katika ushindi uliowaweka alama moja pekee nyuma ya vinara Arsenal ambao wao wamecheza mechi moja zaidi.
Guardiola alitoa wito huo kwa masogora wake hususan baada ya kipa wake nambari moja, Ederson, kuondolewa kwa mechi kufuatia jeraha kipindi cha kwanza.
“Si nzuri. Tutafuatilia na daktari ili kuelewa ni kiwango gani,” alithibitisha jeraha hilo la bega.
Hapa kwa hapa
Ushindi wa Man-City uliwazolea alama hadi 79 baada ya mechi 34 hivyo wana mechi moja ya akiba.
Mabingwa hao watetezi walihitaji kujibu ushindi wa Arsenal dhidi ya Spurs katika mechi iliyotangulia Jumapili, ubabe ambao uliwafanya kunata kileleni kwa alama 80 baada ya mechi za raundi ya 35 wikendi zikisalia tatu pekee EPL ifike tamati.
Awali Jumamosi, Liverpool ya kocha Jurgen Klopp iliona vimulimuli ugenini ikidondosha pointi kwa mara nyingine katika sare ya 2-2 na West Ham kufuatia kichapo cha 2-0 mikononi mwa wenyeji Everton, na sasa ni wazi wamejitoa kwenye mbio za kubeba EPL.
Zikisalia mechi tatu pekee rasmi ligi itamatike, ubashiri wa Arsenal kushinda ligi umeongezeka kwa asilimia 6% kwa mujibu wa wachanganuzi data wa Opta baada ya ushindi wao dhidi ya mahasimu Spurs huku wa Liverpool ukiporomoka hadi asilimia 0.1%.
Hata hivyo, Opta bado inawaweka Man-City kifua mbele kunyanyua EPL na asilimia 67%.
Silva kuondoka Chelsea
Wakati huo huo, Thiago Silva ataondoka Chelsea mwishoni mwa msimu huu.
Silva, 39, alijiunga na Blues akiwa mchezaji huru kutoka PSG mnamo Agosti 2020.
Amecheza mechi 151 akishinda Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Klabu Bingwa Duniani na kombe la UEFA Super Cup.
“Nilikuja hapa kwa nia ya kukaa mwaka mmoja tu ikaishia kuwa minne,” Silva alisema kuwaaga mashabiki wa Blues.
PSG mabingwa wa Ligue 1
Kwingineko, Paris Saint-Germain Jumapili walishinda taji lao la tatu mfululizo la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) baada ya namba mbili Monaco kulazwa 3-2 na Lyon.
PSG wako mbele kwa pointi 12 na Monaco hawawezi kuwafikia zikisalia mechi tatu pekee ligi ifike kikomo.
Ni taji la 12 la mabwanyenye hao wa Ligue 1 na la 10 katika kipindi miaka 11 iliyopita.
Masogora wa Luis Enrique sasa wataelekeza macho UEFA watakapomenyana na Borussia Dortmund katika nusu-fainali mwezi ujao.