Fahamu magonjwa yanayoweza kuenea kwa kasi msimu huu wa mafuriko nchini
NA WANGU KANURI
KWA wiki kadhaa sasa, tumekuwa tukishuhudia mvua kubwa ambayo imesababisha majanga tofauti nchini.
Angalau watu 70 wamepoteza maisha yao huku maelfu ya wengine wakibaki bila makao kwa mujibu wa idadi iliyohesabiwa wikendi.
Mvua hii ambayo imeendelea kunyesha, imesababisha pia mmomonyoko wa udongo, mito ikavuja kingo zake na barabara zikaharibiwa.
Huku Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa likishauri Wakenya kuwa mvua itaendelea kunyesha na kusababisha madhara zaidi, haya ni baadhi ya magonjwa ambayo yanaweza kuenea kwa sababu ya mafuriko na mvua nyingi.
Magonjwa haya huenea kwa kunywa maji chafu, kugusa kwa kuoga mwili au kuosha nguo na maji hayo chafu na kuwepo kwenye mazingira yenye maji haya chafu.
Kwa mfano; unapokunywa maji chafu, upo kwenye hatari ya kuugua ugonjwa wa kuendesha (diarrhoea), homa ya matumbo (typhoid), ugonjwa wa kupooza (poliomyelitis), na nimonia inayosababisha na bakteria ya legionella (legionellosis).
Data ya 2019 ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliratibu kuwa watu milioni 9 huugua kutoka homa ya matumbo huku watu 110,000 wakifariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.
Homa ya Matumbo
Dalili za homa ya matumbo ni pamoja na kuhisi joto jingi, uchovu, kuwa na maumivu ya kichwa na tumbo, kuhisi kichefuchefu, kuendesha au kukaukiwa na choo.
Isitoshe, mwaka huu, WHO ilitangaza kuwa ugonjwa wa kuendesha kwa watoto ndio ulikuwa wa tatu kwa kuongoza kwa vifo kwa watoto walio na umri wa miaka 5.
Kila mwaka ugonjwa huo uliwaua watoto 443,832 huku wengine 50,851 wakiwa watoto walio na umi wa miaka 5 hadi 9. Duniani kuna visa bilioni 1.7 za watoto wanaougua ugonjwa wa kuendesha kila mwaka.
Unapooga au kuosha nguo na maji haya chau, basi upo kwenye hatari ya kuugua ugonjwa wa kuendesha damu (bacillary dysentery), na ugonjwa wa macho unaoenezwa na bakteria ya Chlamydia trachomatis (trachoma).
Data ya mwaka wa 2022, ilionyesha kuwa watu milioni 125 wanaishi na ugonjwa wa trakoma huku wakiwa kwenye hatari ya kuwa vipofu.
Magonjwa yanayoenezwa na wadudu
Isitoshe, wadudu huzaana kwenye maji haya na kusababisha magonjwa kama malaria, yale yanayoenezwa na mbu lakini husababisha madhara kwenye akili ya mtu (West Nile Fever) na maambukizi yanayosababishwa na viroboto vidogo vinavyochimba ndani ya ngozi na kutaga mayai huku mgonjwa akihisi mwasho mkali na anapata vipele (scabies).
WHO limeeleza kuwa ugonjwa wa upele huathiri zaidi ya watu milioni 200 maishani mwao huku wengine milioni 400 wakiathiriwa kwa mwaka. Huku watu wengi wakivamiwa na viroboto 10 hadi 15, dalili za scabies ni pamoja na kuhisi kujikuna sana haswa usiku, kuvimba kwenye vidole, nyonga, mikono, miguu, matiti na sehemu za siri kwa wanaume.
Hali kadhalika dalili za West Nile Fever ni pamoja na kuhisi joto jingi na uchovu, kuwa na maumivu ya kichwa na mwili, kichefuchefu, kutapika na kuwa na vipele kwenye ngozi.
Kwa mujibu wa data ya malaria ya 2022, visa milioni 249 vilishuhudiwa huku vifo 608,000 vikirekodiwa katika nchi 85 ikiwemo Kenya. Watoto walio chini ya miaka 5 ndio walichangia sana idadi ya vifo kwa asilimia 80 (486,400).
Dalili za Malaria
Dalili za malaria huanza kuonekana baada ya siku 10-15 ya kuumwa na mbu na ni pamoja na kuhisi joto jingi, kuwa na maumivu ya kichwa na kuhisi kama unatetemeka.
Pia, kunayo magonjwa yanayoenezwa baada ya maji kuchafuliwa na mkojo na mavi ya wanyama au wanadamu (schistosomiasis). Angalau watu milioni 251.4 walihitaji kutibiwa dhidi ya schistosomiasis mwaka wa 2021.
Magonjwa yanayoathiri upumuaji
Baada ya mvua nyingi, nyumba nyingi bado huwa na unyevunyevu na huweza kuhatarisha magonjwa kadha wa kadha yakiwemo ugonjwa wa pumu, nimonia, kukohoa kwingi na kupiga chafya hivi kuathiri mapafu.
Mwaka wa 2019, ugonjwa wa pumu uliathiri watu milioni 262 huku vifo 455,000 vikirekodiwa. Dalili zake ni pamoja na kukohoa, kukosa hewa, na kuhisi kifua kikiwa kimefungana.
Asilimia kubwa ya nimonia huwaathiri watoto huku dalili zake zikiwemo kukohoa, kukosa hewa, kuhisi joto jingi, kutetemeka, kutokwa na jasho, kuhisi kutapika, kuendesha na kutapika, kuhisi uchovu na kuhisi kifua kimefungana.