TAHARIRI: Serikali izidishe tahadhari zake kufaa wananchi
USIKU wa kuamkia Jumatatu kulikuwa na matukio mawili makuu nchini ambayo yalionyesha kwamba bado ipo mianya ambayo serikali inafaa kuziba ili kuepuka madhara zaidi kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini.
Mwanzo, wazazi na wanafunzi waliamkia habari za kushtukiza kwamba shule hazitafunguliwa hadi tarehe sita yaani Jumatatu ijayo.
Tangazo hili lilitolewa na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu akisema kwamba uamuzi huu ulifanywa baada ya kufanya tathmini ya hali ilivyo nchini kutokana na athari za mafuriko.
Si tangazo lenyewe lililokera wadau katika elimu bali wakati ambapo lilitolewa. Tangazo hili lilitolewa usiku wa manane. Tangazo hili likitolewa na Wizara ya Elimu, tayari kulikuwa na maelfu ya wanafunzi wanaoishi kaunti za mbali kabisa na shule zao, ambao tayari walikuwa wameabiri magari kuenda shuleni.
Ilikuwa adha kwa wazazi waliokuwa wamelipia wanao nauli kuenda shuleni pamoja na usumbufu kwa wanafunzi waliosafiri. Aidha, katika miji mingi wanafunzi wenye mshangao walionekana kukwama baada ya kupata tangazo hili huku wakiwa tayari wametoka nyumbani.
Baadhi yao waliishia kurandaranda tu mijini wasijue la kufanya.
Mafadhaiko hayo ya wazazi, wanafunzi na walimu yangeweza kuepukwa iwapo Wizara ya Elimu ingetoa tangazo hili kwa wakati ufaao.
Hii ni kwa sababu si eti kwamba serikali haikufahamu hali ya mafuriko nchini! Mkorogo wa mambo katika Wizara ya Elimu hapo Jumatatu ulianika tu kukosekana kwa mpangilio miongoni mwa wadau katika sekta ya Elimu.
Baada ya hayo ya Waziri Machogu, taifa la Kenya liliamkia habari nyingine za kuatua moyo. Nchi ilipoteza zaidi ya watu 46 waliothibitishwa kufikia Jumatatu jioni katika mkasa mwingine wa mafuriko eneo la Maai Mahiu.
Maji mengi ambayo yalidaiwa kuzuiliwa katika dimbwi yalivunja kingo na kufagia makazi ya watu usiku wenyeji wakiwa wamelala.
Mamia ya watu wengi katika pembe mbalimbali za nchi pia waliendelea kuathiriwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi.Serikali iliungama kwamba kufikia sasa kaunti zote 47 zimeathiriwa na mafuriko.
Zaidi ya serikali kutoa matangazo kuhusu hatari ya mafuriko, hatua madhubuti zinafaa kuchukuliwa kunusuru watu kuendelea kupoteza maisha na mali. Ipo haja kwa serikali kutumia maafisa wake wa nyanjani kama vile machifu katika vijiji vyote kuhakikisha kwamba raia wanazingatia tahadhari zinazotolewa.
Umma pia una jukumu la kujua kwamba mvua ya sasa si lelemama na hivyo kila mmoja achukue hatua za kuhakikisha ndugu na jamaa wote wako salama.