Wanafunzi 18 wa MKU kushiriki shindano la kimataifa la Huawei
NA LAWRENCE ONGARO
WANAFUNZI 18 wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) watashiriki shindano la kimataifa la Huawei nchini China mnamo Mei 2024.
Kwenye ziara hiyo, mwanafunzi stadi wa maswala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) katika MKU, Daniel Ochola, atawaongoza wenzake 17.
Waliteuliwa hivi majuzi baada ya kushiriki tuzo za Kusini mwa Afrika zilizofanyika Machi 15, 2024 jijini Nairobi ambapo Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alihudhuria.
Bw Ochola aliibuka miongoni mwa wanafunzi tatu-bora katika uwaniaji wa tuzo hizo.
Jumla ya wanafunzi 21 kutoka Kenya walituzwa vyeti miongoni mwa wanafunzi 6,000 waliojitokeza katika mashindano hayo ya Huawei ICT yaliyofanyika jijini Nairobi.
Bw Ochola alisema alikuwa na ari ya kujifunza maswala ya teknolojia na ndio maana akatia bidii na kuibuka mshindi na kuteuliwa kuwa mmoja wa wanafunzi stadi.
“Kulikuwa na ushindani mkali kutoka maeneo tofauti na tukajipata nyuma ya kikosi cha Nigeria,” akasema Bw Ochola.
Naye afisa kutoka MKU, Bw John Kamau, alisema Bw Ochola ni mwanafunzi mwenye maono na ndio sababu aliweza kupiga hatua hiyo.
“Sisi kutoka chuo cha MKU tunapongeza juhudi zake za kukiweka chuo kwenye ramani ya ulimwengu,” alisema Bw Kamau.
Hapa mchini Kenya kampuni ya Huawei imebuni taasisi za mafunzo ya ICT kwa vyuo 50 kwa kuhakikisha wanapatikana wanafunzi wengi wanaoelewa maswala ya teknolojia.
Wakati huo huo, Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) kiliandaa kongamano la maswala ya kawi ambalo washiriki wake walitoka katika vyuo vikuu vinne.
Kongamano hilo lilijumuisha wanafunzi na wafanyakazi kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, KU, MKU na Chuo Kikuu cha Albert Ludwin cha nchini Ujerumani.
Kulingana na mtaalamu wa maswala ya ubunifu katika masomo ya teknolojia Dkt Donatus Njoroge, ni muhimu kwa wanafunzi kujiongezea ujuzi zaidi katika sekta za kawi safi na teknolojia.