Habari za Kitaifa

Mafuriko: Barabara ya kuunganisha Kenya na Sudan Kusini yakatika

April 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA OSCAR KAKAI

SHUGHULI za uchukuzi zimetatizika kwenye barabara inayounganisha Kenya na taifa jirani la Sudan Kusini huku wasafiri wakihofia mashambulio kutoka kwa majangili.

Barabara kuu ya Kitale–Kapenguria-Lodwar–Juba imekatika karibu na soko la Lous katika Kaunti ya Pokot Magharibi kufuatia mvua kubwa inayonyesha katika eneo hilo na sehemu nyingine za nchi.

Barabara hiyo kuu ndio ya pekee inayounganisha kaunti ya Turkana na maeneo mengine ya Kenya. Aidha inaingia Turkana na kufululiza hadi nchini Sudan Kusini.

Wasafiri kwenye barabara hiyo sasa wanahofia kuwa huenda majangili wakawavamia katika eneo hilo ambalo hushuhudia mashambulio mengi.

Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa mrundiko wa magari huku usafiri ukikwama.

Wasafiri wakiwa wamekwamba baada ya barabara kuu ya Kitale–Kapenguria-Lodwar–Juba kukatika karibu na soko la Lous katika Kaunti ya Pokot Magharibi kufuatia mvua kubwa inayonyesha. PICHA | OSCAR KAKAI

Mvua kubwa iliyonyesha Jumapili usiku imeathiri watumiaji wa barabara hiyo na hata vituo vya kibiashara kama Kainuk, Lokichar, Lodwar, Kakuma na Lokichoggio.

Maeneo hayo hutegemea miji ya Kitale na Kapenguria kupata matunda, unga, na mboga.

Baadhi ya wasafiri wamekuwa wakilala barabarani kutokana na mafuriko.

Mabw Mohamed Waswa na Peter Eboya ambao walikuwa wakielekea mjini Lodwar kutoka Kitale na Eldoret mtawalia, walisema Jumanne kuwa huenda majangili wakatumia nafasi hiyo kushambulia wasafiri.

Kamishina wa Kaunti ya Pokot Magharibi Khalif Abdulahi alisema kuwa hali hiyo ni mbaya na ilimlazimu kuingilia kati ili kuhakikisha polisi wanatumwa hapo kuwalinda wasafiri.

“Nilipopokea ripoti na nikahakikisha maafisa kutoka kituo cha polisi cha Marich wanafika hapo kupiga doria,” akasema Bw Abdulahi.

Alisisitiza haja ya kuondoa mrundiko wa magari na kupeana njia mbadala ili kuokoa wasafiri ambao wanaumia.

“Tunaelewa hali ni mbaya lakini tunajaribu kutatua shida hiyo. Mwanzo kipaumbele kiko kwa usalama wa wasafiri ambao wamekwama kwenye barabara,” akasema.

Bw Abdulahi aliwataka wasafiri kuwa na utulivu.

Kamishina huyo aliwakikishia wakazi kuwa atakuwa akipeana habari za mara kwa mara kuhusu suala hilo.

Uchunguzi unaonyesha kuwa juhudi za kukarabarati eneo hilo zimeanza kutekelezwa na maafisa wa dharura pamoja na mwanakandarasi wa barabara inayojengwa ya Marich-Kopass.

Wasafiri ambao wamekwama kwenye barabara hiyo waliambia Taifa Leo kwamba kuna hatari ya kukatika zaidi.

“Ni mbaya sana. Tulikuwa tunaenda biashara mjini Lodwar lakini sasa tumekwama hapa,” akasema Bw John Kiptum, msafiri.

Naibu Chifu wa kata ya Kosetei Joseph Siwa ambaye alitumia barabara hiyo, anaitaka serikali kupitia kwa Halmashauri ya Barabara Kuu nchini (KeNHA) kuzuru eneo hilo kabla ya kuharibika zaidi.

“Tunaomba serikali iingilie kati kuziba mashimo kwenye barabara,” akasema Bw Siwa.

Aliitaka serikali kuu na ya kaunti kuchukulia suala hilo kwa uzito na kwa dharura.

Haya yanajiri baada ya mafuriko kusomba vijiji vya eneo la Kambi Karai mnamo Jumatano wiki jana na kusababisha hasara kubwa kutokana na mvua kubwa inayonyesha katika eneo hilo.

Wasafiri wakiwa wamekwamba baada ya barabara kuu ya Kitale–Kapenguria-Lodwar–Juba kukatika karibu na soko la Lous katika Kaunti ya Pokot Magharibi kufuatia mvua kubwa inayonyesha. PICHA | OSCAR KAKAI

Maeneo mengine ambapo uchukuzi umeathirika ni Kalemngorok, Kainuk, Lokichar, Karoge, Kasuroi kwenye barabara ya Lodwar – Lokichar.

KeNHA imetoa tahadhari ikiwataka wasafiri kwenye barabara ya Lodwar-Lokichar kujihadhari wanapofika maeneo ya Karoge na Kasuroi.

“Mvua ya hivi majuzi imeharibi sehemu za barabara na daraja la Lokichar. Ukarabati bado unaendelea na waendeshaji magari wanafaa kuenda polepole na kufuata maagizo,” KeNHA ikasema.

Mkazi wa Kalemngorok Esther Ajuma, anasema kuwa mji wa Lodwar na mingine hutegemea kaunti za Trans Nzoia na Uasin Gishu kupata bidhaa muhimu na bila daraja eneo la Kalemngorok, itakuwa shida kubwa.

Bi Ajuma anasema kuwa eneo hilo ni la ujangli na wakati mto huo hufurika kutoka mji wa Lodwar, husababisha hasara kubwa na huduma kukatika.

Bw James Kisike, mkazi mwingine, anasema kuwa wamekuwa wakilalamikia hali hiyo kwa KeNHA wakiitaka ijenge barabara.

“Tunahitaji barabara ili isaidie kwa kushika doria hasa wakati wa mashambulio,” akasema Bw Kisike.

[email protected]