Makala

Je, wafahamu kwamba mikoko ina matunda? Ila si mikoko yote!

May 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

MWAMBAO wa Pwani unafahamika sana kwa kuwa na msitu wa mikoko kutokana na kwamba eneo hilo linapakana na Bahari Hindi.

Ikumbukwe kuwa mikoko ni aina za miti au vichaka vinavyokua katika maji ya chumvi, hasa kwenye fukwe za bahari za kanda za trokipi.

Kwa wale waliobahatika kuujua mkoko wanafahamu fika kuwa mti huo huzaa au kutoa mbegu maalumu zinazoitwa mbegu za mikoko.

Mbegu hizo huwa zimeshabihiana na vijiti virefuvirefu.

Mbegu hizi kubwa za kijani zina urefu tofauti wa kuanzia sentimita 10 hadi 40.

Mbegu za mikoko mara nyingi huchipua kwa kutoa miche ya mikoko zikiwa bado zinaning’inia juu ya mti, kisha miche hii hudondoka kwenye udongo au bahari chini (ya mti) na kuanza kuota moja kwa moja.

Ifahamike kwamba mbegu hizi za mikoko pia zinaweza kuishi kwa miezi mingi na kusafiri masafa marefu baharini kabla ya kufika kwenye udongo na kuanza kuota mizizi huku ikikua na kuwa miche na kisha mti kamili.

Huku ukiyatafakari hayo, je, wajua pia kwamba kuna mikoko mingine inayozaa matunda?

Wataalamu waliohojiwa na Taifa Leo walifichua kuwepo kwa aina nyingine ya mikoko iliyo nadra kupatikana, hasa Pwani lakini ambayo ina uwezo wa kuzaa matunda.

Bi Husna Bakari, mkazi wa Kisiwa cha Pate, Lamu Mashariki, akionyesha mbegu ya kawaida ya mkoko ambayo huwa kijani kibichi na ndefu kama kijiti cha kati ya sentimita 10 hadi 40. PICHA | KALUME KAZUNGU

Mikoko yenyewe inaitwa Mikomafi.

Aghalabu kuna ‘Mkomafi‘ ambao kwa jina la Kisayansi unajulikana kama Xylocarpus granatum na ‘Mkomafi dume,’ kwa jina la Kisayansi ukifahamika kuwa Xylocarpus moluccensis.

Kinyume na mikoko mingine ya kawaida, Mikomafi huwa haimei na kukua kwa urahisi hadi kufikia ukubwani.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Afisa Mtafiti wa Mikoko na Masuala ya Uhifadhi katika Shirika la Wetlands International, Bi Shawlet Cherono alisema ni bayana kwamba wengi wa wanaoendeleza upanzi wa mikoko Lamu na Pwani wamekuwa wakikwepa kabisa kupanda Mkomafi na Mkomafi dume, hali ambayo inaacha aina hiyo ya mikoko kuwa kwenye hatari kubwa ya kuangamia.

Miongoni mwa sababu zinazosukuma wahifadhi wengi kuepuka kupanda Mkomafi na Mkomafi dume ambayo huzaa matunda ni jinsi aina hiyo ya mikoko ilivyo migumu kupatikana, hasa mbegu zake.

Bi Cherono alisema ni wazi wanaojihusisha na uhifadhi wa mikoko wametelekeza upanzi wa aina ya Mkomafi na Mkomafi dume.

Afisa Mtafiti wa Masuala ya Uhifadhi katika Shirika la Wetlands International, Bi Shawlet Cherono akionyesha miche ya Mkomafi iliyofaulu kupandwa na kuoteshwa eneo la Pate, Lamu Mashariki. Mkomafi ni miongoni mwa mikoko inayozaa matunda. PICHA | KALUME KAZUNGU

Alisema yote yanatokana na gharama inayohusishwa na aina hiyo ya mikoko.

“Wengi wanaonelea kuwa rahisi kuokota zile mbegu za kawaida za mikoko ambazo hutapakaa ovyo ovyo kwenye mazingira yao na kupanda. Ni vyema pia tuwajibikie upanzi wa Mkomafi na Mkomafi dume ili kuongeza idadi yake kwenye mazingira yetu,” akasema Bi Cherono.

Je, mikoko hii ya Mkomafi na Mkomafi dume hupandwa vipi?

Kwanza, matunda yanayozaliwa na mikomafi huwa na magamba magumu.

Magamba hayo huhifadhi mbegu kubwakubwa mithili ya kokwa ya embe ndani.

Kuzifikia mbegu hizi lazima mja apasue tunda hilo gumu la mkomafi.

Mbegu hutolewa na kisha kuanikwa kwa muda juani.

Ni mbegu hizo ambazo zinatumiwa kwanza kwa kupandwa kwenye eneo maalumu lililotengwa, yaani nursery, kabla ya kuhamishiwa sehemu inayohitajika ya upanzi.

Ni kutokana na mpangilio mrefu wa kupanda na kukuza mkomafi ambapo idadi ya aina hiyo ya mikoko imesalia kuwa finyu.

Aidha wataalamu wa uhifadhi wa mazingira wanahimiza waendelezaji upanzi wa miti, hasa mikoko kuzingatia kupanda kwa wingi Mkomafi na Mkomafi dume ili isiangamie au kupotea kabisa kwenye mazingira yao.

Ikumbukwe kuwa Kenya iko na karibu aina tisa za mikoko inayotambulika kwenye mazingira oevu kote ulimwenguni.

Kati ya hizo, ni Mkomafi na Mkomafi dume ambayo idadi yake inatambulika kuwa ndogo.

Aina nyingine saba zilizosalia za mikoko, ambazo ndizo zinazopatikana kwa wingi Pwani ya Kenya ni Rhizophora mucronata (Mkoko), Bruguiera gymnorrhiza (Muia), Ceriops tagal (Mkandaa), Sonneratia alba (Mlilana), Avicennia marina (Mchu), Lumnitzera racemosa (Kikandaa) na Heritiera littoralis (Msindukazi).

Bi Swabra Musa,41, mmoja wa akina mama tajika wanaojihusisha na upanzi na uhifadhi wa misitu ya mikoko Lamu, aliomba kuwepo na mpango wa kuielimisha jamii hasa kuhusiana na kuwepo kwa aina hiyo ya mikoko ambayo idadi yake ni ndogo, jinsi ya kuipanda na kuikuza.

Bi Musa alisema ni wananchi wachache wenye ufahamu kwamba aina hiyo ya mikoko inapatikana, hasa kwenye maeneo kama Lamu.

“Wengi wetu hata hatujui kuhusu Mkomafi na Mkomafi dume. Twajua tu aina nne ambazo hupatikana na kukuzwa kwa wingi eneo letu. Aina hizo ni Mkoko, Muia, Mchu na Mkandaa. Tukipewa hamasa kuhusu Mkomafi na Mkomafi dume na jinsi tutaiandaa kwa upanzi litakuwa jambo zuri,” akasema Bi Musa.

Lamu inaongoza kwa asilimia kubwa ya msitu wa mikoko upatikanao Pwani na kote nchini.

Zaidi ya asilimia 60 ya misitu yote ya mikoko ipatikanayo Kenya iko Lamu.