Wito uteuzi wa makamishna wa IEBC uharakishwe
NA CHARLES WASONGA
VIONGOZI wa kidini wameitaka serikali kuhakikisha kuwa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wanateuliwa kwa wakati ufaao.
Kwenye taarifa iliyotolewa baada ya kukamilika kwa Kongamano la Kitaifa la Mazungumzo katika jumba la Ufungamano, Nairobi, walisema si sawa kwa taifa kusalia kwa miezi 16 bila tume halali ya kuendesha uchaguzi.
Tayari eneobunge la Banissa halina mbunge na wadi nne za Nyamaiwa, Kisa Mashariki, Lake Zone na Chewena hazina madiwani.
Viongozi hao walieleza kuwa ni kinyume cha Katiba kwa maeneo hayo ya uchaguzi kusalia bila wawakilishi.
“Aidha, kaunti ya Kisii haina Naibu Gavana kwa sababu hakuna tume ya kuchapisha jina la mteule mpya wa wadhifa huo,” taarifa yao ikasema.
Taarifa hiyo ilitiwa saini na Katibu Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK) Chris Kinyanjui, Katibu Mkuu wa Baraza la Kuu la Waislamu Nchini (Supkem) Abdullahi Salat na Katibu mkuu wa Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini (KCCB) Simon Peter Kamomoe.
Viongozi hao wa kidini pia walisema kuwa kutokuwepo kwa makamishna wa IEBC kumechangia kutokea kwa mzozo wa kikatiba baada ya makataa ya kubadilishwa kwa mipaka ya maeneo wakilishi.
“Tunamtaka Rais William Ruto, wabunge na wadau wengine kuharakisha mchakato wa uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC. Itakuwa muhimu kutenganisha mchakato huu na mjadala kuhusu siasa kutokana na umuhimu wa tume hii kwa taifa letu,” ikaongeza.
Lengo la mkutano huo ulioshirikisha viongozi wa NCCK, KCCB na Supkem ni kuhusu Mazungumzo kuhusu Hali ya Kitaifa.
Kongamano hilo liliitishwa kujadili ripoti iliyowasilishwa bungeni mnamo Novemba 23, 2023, na Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco) na miswada mingine tisa ya kufanikisha utekelezaji wa ripoti hiyo.
IEBC inaundwa na makamishna saba na Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) ambaye pia huhudumu kama katibu wa tume, ambaye huteuliwa na makamishna hao.
Makamishna hao akiwemo Mwenyekiti, huteuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge.
Kila kamishna huhudumu kwa muhula mmoja wa miaka sita ambao hauwezi kuongezwa.
Wakati huu, tume hiyo haina makamishna na hivyo, haiwezi kutekeleza majukumu yake makuu kama vile kuendesha chaguzi na kuchora upya mipaka ya maeneo-wakilishi.
Muhula wa mwenyekiti wa zamani Wafula Chebukati na makamishna Abdi Guliye na Boya Molu ulikamilika Januari 17, 2023.
Makamishna wengine wanne wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera, walilazimishwa kujiuzulu Desemba 2022 kwa tuhuma za kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa na Bw Chebukati katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 15, 2022.
Aidha viongozi wa kidini pia wanaitaka serikali kuchapisha ripoti ya Nadco kwa namna ambayo itaweza kufikiwa na Wakenya wote “ili waelewe mipango kuhusu mustakabali wao.”
“Aidha, tunatoa wito kwa wabunge kuhakikisha kuwa maoni ya Wakenya wote waliojitokeza yanashirikishwa katika miswada ya kufanikisha utekelezaji wa ripoti ya Nadco,” viongozi hao wa kidini wakaeleza kupitia kwa taarifa hiyo.