Mafuriko: Papa asimama na Kenya
HASSAN WANZALA Na STANLEY NGOTHO
PAPA Francis amesema Jumatano kuwa ameguswa na Wakenya kipindi hiki wakikabiliana na mafuriko ya maafa.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa X (zamani Twitter) kiongozi huyo wa kidini ametoa wito wa maombi maalum kwa waathiriwa wa janga hili la kiasili.
“Ninafuatilia kwa karibu yanayojiri nchini Kenya kipindi hiki raia wakikabiliana na mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu wengi na kuharibu maeneo mengi. Tuombe sote kwa ajili ya wale ambao wanatatizika kufuatia janga hili la kiasili,” ameandika Papa Francis.
Kauli ya Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki inajiri saa chache baada ya miili miwili kuopolewa katika mto wa msimu kufuatia mafuriko Kitengela, Kaunti ya Kajiado huku idadi ya waliopoteza maisha eneo la Mai Mahiu, Kaunti ya Nakuru ikipanda hadi 52 kutoka idadi ya awali ya 46.
Meneja wa Manispaa ya Kitengela Bi Josphine Nashipae amesema kwamba shughuli ya uokoaji inaendelea katika eneo hilo.
Alfajiri ya kuamkia Jumatano, kulisikika kilio cha wakazi wa Kitengela wakiitisha usaidizi baada ya maji ya mafuriko kuzingira nyumba zao.
Mafuriko hayo yalisababisha vifo vya wanaume wawili.
Mto Ilkeek-lemedung’i ambao ni wa msimu ulivunja kingo zake kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na maji yakazingira nyumba za karibu.
Juhudi za uokozi ziliyumbishwa kwa sababu mvua ilikuwa ikinyesha bila kupusa.
Licha ya ugumu huo wa juhudi za uokozi, kufikia Jumatano asubuhi maafisa kutoka shirika la Msalaba Mwekundu–Red Cross—walikuwa wamefanikiwa kuokoa watu 100.
Lakini familia kwa makumi, ziliendelea kulazimika kukaa ndani ya nyumba zao katika majumba ya orofa eneo hilo, maji yakiwa yamezingira kila upande.
Kufikia mchana, waokoaji wameendelea kutumia maboti kuokoa waathiriwa.
Bi Jane Kamau, mkazi wa Newvalley, Kitengela ni mmojawapo wa waliookolewa.
“Nilikuwa nimekwama nyumbani nikiwa na watoto wangu watatu. Tulipanda juu ya nyumba yetu tulipoona mafuriko yakiongezeka. Nina furaha kwamba tumenusurika,” akasema Bi Kamau.
Mkazi mwingine, Bw Joseph Kinuthia, amesema amepoteza karibu kila kitu, kuanzia kwa mavazi hadi kwa chakula.
Amesema kila kukinyesha mvua nyingi, wakazi wa eneo hilo huathirika vibaya.
“Wenzangu hapa watarajie hali kuwa mbaya zaidi endapo mvua itaongezeka,” akasema Bw Kinuthia.
Mwili wa kwanza umepatikana saa sita na nusu mchana katika mto wa msimu wa Noonkopir, ikishukiwa mwendazake alifagiliwa na maji ya mafuriko akijaribu kuvuka daraja usiku.
Ulipatikana mita 200 kutoka kwa daraja lakini pikipiki yake haikupatikana. Mke wa marehemu alitambua mwili huo.
“Hakurudi nyumbani kutoka kazini Jumanne na ninasikitika kuwa ameaga dunia,” akasema mjane huyo huku akilia.
Mwili wa pili ulipatikana kwa mtaro wa majitaka unaoelekeza maji kwa mto wa msimu ulioko karibu na gereza la Kitengela GK.
Bi Nashipae amewataka wakazi wanaoishi katika maeneo ya nyanda za chini kuhamia katika maeneo ya nyanda za juu kuepuka maafa.