Habari za Kitaifa

Wazee wana uwezo kuzuia mvua – Atwoli

May 1st, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Cotu-K) Francis Atwoli ameibua kicheko wakati wa sherehe za Leba Dei katika bustani ya Uhuru Gardens, Nairobi, alipoelezea sababu ya mvua kutonyesha kuvuruga sherehe hizo.

Bw Atwoli alisema alipata hakikisho kutoka kwa mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba kwamba mababu zake wamezuia mvua kunyesha “ili sherehe ziendelee bila kuvurugika”.

“Ningetaka kuwahakikishia nyote mlioko hapa kwamba mvua haitanyesha kwa sababu tulimtuma mmoja wetu, Bw Omboko Milemba aongee na mababu zake kule anakotoa wazuie mvua isinyeshe. Wanao uwezo wa kusimamisha mvua isinyeshe,” Bw Atwoli akasema huku waliohudhuria sherehe hizo–akiwemo Rais William Ruto–wakicheka.

Bw Milemba, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet), anatoka jamii ya Abanyore wanaoishi Kaunti ya Vihiga.

Inaaminika kuwa kuna baadhi ya watu, hasa wazee, wa jamii hiyo wenye uwezo wa kutumia ‘mazingaombwe’ kuzuia mvua kunyesha endapo kuna sherehe maalum.

Wakati huu mvua inanyesha kwa wingi katika kaunti ya Nairobi na maeneo mengine nchini.

Mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyotokana na mvua hiyo yamesababisha maafa na uharibifu mkubwa wa mali.

Katika Kaunti ya Nairobi, mvua iliendelea kunyesha usiku wa kuamkia Jumatano licha ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Dkt David Gikungu kutangaza kuwa itaanza kupungua katika wiki hii.