Habari za Kitaifa

Linturi pabaya hoja ya kumtimua ikipita Bungeni

May 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa limepitisha hoja ya kumtimua afisini Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na kutoa nafasi ya kuundwa kwa kamati maalum ya wabunge 11 kuchunguza madai dhidi yake na kuandaa ripoti.

Kwenye matokeo ya kura iliyopigwa kielektroniki mnamo Alhamisi adhuhuri, jumla ya wabunge 149 waliunga mkono hoja hiyo na 36 wakaipinga.

“Matokeo ya upigaji kura ni kama yafuatayo. Wale waliopiga kura ya NDIO kuunga mkono hoja hii ni 149 na wale waliopiga kura ya LA kuipinga ni 36. Kwa hivyo, hoja hiyo imepita baada ya kutimiza hitaji la kuungwa mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge walioko bungeni na walipiga kura,” akasema Spika Moses Wetang’ula.

“Hatua hiyo sasa inatoa nafasi ya kuundwa kwa kamati maalum ya wabunge 11 kuchunguza madai hayo na kuwasilisha ripoti katika Bunge hili baada ya siku 10. Wanachama wa kamati hiyo watateuliwa ifuatavyo. Mrengo wa wengi utawasilisha majina sita, mrengo wa wachache utawasilisha majina manne na chama cha Jubilee kitawasilisha jina moja,” akaongeza.

Hoja hiyo ilikuwa imedhaminiwa na Mbunge wa Bumula Jack Wamboka Wanami ambaye alimhusisha waziri Linturi na sakata ya uuzaji wa mbolea feki chini ya mpango wa serikali wa utoaji mbolea ya ruzuku kwa wakulima.

Spika Wetang’ula aliamuru kwamba majina hayo ya wabunge 11 yawasilishwe kwa afisi yake kufikia saa saba na dakika 45 mchana Alhamisi.

Baadaye, wabunge watajadili majina hayo na kuyaidhinisha au kuyakataa, wakati wa kikao cha alasiri kuanzia saa nane na nusu mchana.

Bw Linturi ndiye Waziri wa kwanza kujipata katika hali hii ya kukataliwa na wabunge, tangu serikali ya Kenya Kwanza ilipoingia mamlakani Septemba 13, 2022.