Habari za Kitaifa

Mabasi ya Kensilver, Mbukinya, Moline, Wamasaa yapigwa marufuku barabarani

May 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANDISHI WETU

IDARA ya Usalama barabarani NTSA limefutilia mbali leseni za kampuni 64 za magari ya uchukuzi baada ya kugunduliwa hayajatimiza vigezo hitajika vya kiusalama.

Miongoni mwa kampuni hizo ni ile ya Kensilver, Mbukinya, Moline, Wamasaa, Kiambu United na Moro Express.

Kulingana na taarifa iliyotumwa kwenye akaunti ya mtandao wa kijamii wa X wa NTSA, umma unashauriwa kuepuka kuabiri magari ya kampuni hizo zilizotajwa kwenye orodha ndefu.

Magari ya Kensilver huhudumu Nairobi, Maua, Embu, Meru huku yale ya Mbukinya yakihudumu Nairobi, Nakuru, Kapsabet, Chavakali, Butere, Lwanda, Busia, Kericho, Sondu, Katiko, Homabay na Mbita. Yale ya Moline huhudumu Nairobi, Nakuru, Eldoret, Kitale, Kericho, Kisumu, Busia na yale ya Wamasaa yakihudumu Mombasa, Machakos, Kitengela, Namanga, Nyamira, Kisii, Migori, Sirare, Athiriver, Kitui, Kajiado miongoni mwa miji mingine.

“Polisi wameshauriwa kunasa magari yoyote kutoka kampuni hizi ambayo yatapatikana yakihudumu licha ya leseni zao kufutwa,” ikasema taarifa hiyo.