Habari za Kitaifa

Uchaguzi wa UDA kufanywa tena katika vituo 538

May 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MOSES NYAMORI

CHAMA tawala cha Rais William Ruto, United Democratic Alliance (UDA) kimeagiza uchaguzi mashinani ufanywe tena Jumamosi katika vituo 538 vya kupigia kura.

Hii ni baada ya uchaguzi uliofanywa Ijumaa wiki jana kukumbwa na changamoto kadhaa ikiwemo mafuriko na vifaa vya kupiga kura kukosa kufika kwenye vituo kwa wakati.

Uchaguzi huo ulifanywa katika kaunti tano zikiwemo Nairobi, Narok, Pokot Magharibi, Busia na Homa Bay.

Kando na hitilafu hizo, wapiga kura pia walilalamika kuwa uchaguzi haukuanza kwa wakati kutokana na mvua inayoshuhudiwa nchini na kwamba baadhi ya wapiga kura walikosa majina kwenye sajili.

Mnamo Jumatano, mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa inayosimamia uchaguzi wa chama cha UDA, (NEB), Bw Anthony Mwaura, alidai kuwa uchaguzi huo ulifanyika bila hitilafu katika baadhi ya vituo.

Katika Kaunti ya Busia, uchaguzi huo utafanywa tena katika vituo 25 ilhali katika eneo la Pokot Magharibi, uchaguzi huo utafanywa tena katika vituo 385. Katika Kaunti ya Nairobi, uchaguzi huo utafanywa tena katika vituo 50 na Narok, katika vituo 70.

“Tunafurahi kwa kuwa uchaguzi ulifanyika katika baadhi ya vituo na watu wakajitokeza kuchagua wawakilishi wao. Hata hivyo, uchaguzi huo haukuweza kufanyika katika vituo vingine kwa sababu mbalimbali na hii ndio maana tumeamua uchaguzi huo ufanywe tena,” akasema Bw Mwaura.

Kwa upande mwingine Bw Mwaura alisema kwamba bodi ya uchaguzi haikuweza kufikia maeneo kadhaa katika Kaunti za Pokot Magharibi na Narok, hasa kutokana na mvua iliyosababisha mafuriko.

Bodi pia iliripoti matukio mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kesi ambapo vifaa vya uchaguzi viliibwa au kuharibiwa. Alisema uchunguzi unaendelea kuhusiana na kesi hizo.

Watu walipiga kura kuwachagua wawakilishi watatu wa vikundi vya kidini, wafanyabiashara (4), wataalamu (3), vijana (4), makundi ya watu wanaoishi na ulemavu (1), wakulima (3) pamoja na wanachama wawili -mwanamke na mwanamume.

Wakati huo huo, Kamati ya Kutatua Mizozo ya Uchaguzi na Uteuzi (ENDR) ya chama hicho, ilitangaza kuwa inachunguza migogoro 209 iliyotokana na zoezi hilo.