Ubabe wa kisiasa wa Gachagua na Ndindi Nyoro wachipuka upya
NA MWANGI MUIRURI
VITA vya kiubabe katika siasa za Mlima Kenya kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro vimerejea, kwa safari nyingine tena vikivumishwa katika Kaunti ya Murang’a.
Kaunti hii imekuwa mwiba sugu wa siasa za Bw Gachagua ambapo kila mara kiongozi akitaka kumwelekezea siasa za upinzani, huwa anaruka hadi Murang’a.
Mnamo Jumanne wiki hii, Bw Gachagua na Bw Nyoro walimenyana miereka katika eneobunge la Mathioya ambapo walitandaza siasa zao kinzani kupitia ziara kuwafaa waathiriwa wa mafuriko yaliyokuwa yameua watu saba.
Baada ya Bw Nyoro kufika na kutoa mchango wake wa Sh2 milioni ambapo alisema Sh1 milioni zilikuwa mchango wa Rais William Ruto, Bw Gachagua alitua eneo hilo saa chache baadaye na akatoa mchango wake binafsi wa Sh1 milioni pamoja na mablanketi.
Katika hotuba yake, Bw Nyoro alisema kwamba alikuwa amefika katika eneo hilo kama kiongozi wa Murang’a aliye na uaminifu kwa Rais Ruto, wale alioandamana nao wakimsifu kama bingwa wa siasa za eneo hilo.
Seneta Joe Nyutu ndiye aliyedhihirisha waziwazi nia ya ziara hiyo ambapo alisema “tumemleta Bw Nyoro hapa kama ishara kwamba yeye ndiye tu kiongozi wa Mlima Kenya anayetujali na nyinyi pia muwe mnamuweka katika mawazo yenu kama kinara wetu Mlima Kenya”.
Bw Nyoro aliandamana pia na mbunge wa Mathioya Edwin Mugo na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Betty Maina.
Baada ya Bw Nyoro kutoka eneo hilo, Bw Gachagua aliyekuwa akihudhuria mazishi ya Askofu Mkuu wa Nne wa Kanisa la AIPCA marehemu Mathenge Kabuthu katika Kaunti ya Nyeri, alitua eneo hilo la Mathioya mwendo wa saa kumi na moja jioni.
Aliandamana na wabunge kutoka Kaunti ya Nyeri, lakini wote wa Murang’a wakikwepa hafla hiyo.
Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata hakuwepo kwenye mkutano wa Bw Nyoro lakini alijitokeza katika mkutano wa Bw Gachagua.
Kama hali ya tahadhari, Bw Kang’ata alikuwa amemtuma mwandani na msaidizi wake Bw Manoah Gachucha ambaye ndiye Waziri wa Masuala ya Vijana na Utaamaduni wa Murang’a kumwakilisha katika mkutano wa Bw Nyoro.
Aidha, Bw Kang’ata alikuwa ameandaa ziara yake mnamo Jumatatu mchana na kujipigia debe kivyake kama aliyejali waathiriwa hao wa janga lililowazika watu katika eneo hilo wakiwa hai vitandani mwao wakiwa wamelala mwendo wa saa saba usiku. Hii ni baada ya maporomoko ya ardhi kutokea na kuwalalia.
Katika hotuba yake, Bw Gachagua alilalamika kwamba amekuwa akikosa mwanya wa kutembelea maeneo kadha ya Murang’a kutokana na kukosa wa kumwalika na kumlaki.
Diwani wa Gitugi Edwin Mwangi ndiye aliyejitokeza kama kiongozi mwenyeji kumlaki Bw Gachagua, hali iliyomsononesha (Bw Gachagua) kiasi kwamba alisema “licha ya hawa watu wa Mlima Kenya kunichukulia kama mfalme wao kwa kuwa hakuna mwingine, huwa ninakosa kutimiza matumaini ya watu wangu ya kuwatembelea kwa kukosa wa kunilaki”.
Bw Nyoro huwa hahudhurii mikutano ya Bw Gachagua katika eneo lolote hata Kiharu ikiwa Rais Ruto hayuko katika hafla hizo.
Ni Februari 10, 2024, pekee ambapo wawili hao walihudhuria mkutano mmoja wa kisiasa katika Kaunti ya Murang’a baada ya Rais Ruto kusemwa kuwashurutisha kufanya hivyo kama njia ya kupunguza hisia za uhasama kati yao.
Wandani wao walikuwa wamelumbana kwa wiki mbili mfululizo ambapo hata wito wa Bw Gachagua afutwe kazi, katika uchaguzi wa 2027 asiteuliwe kuwa mgombea mwenza na 2032 asiwe mrithi wa Ikulu, ulikuwa umetolewa na wandani wa Bw Nyoro.
“Mimi ndiye tu ambaye Mlima Kenya wako naye kama kinara. Hawa watu huwa wanatamani niwatembelee mara kwa mara lakini mimi hukosa wa kunialika na kunilaki. Naomba diwani Mwangi awe akinialika hapa Mathioya,” akasema Bw Gachagua katika ziara hii yake ya juzi.
Hata hivyo, Bw Mugo amejitetea kwamba hakuna haja ya Bw Gachagua kuomba kualikwa au kulakiwa kwa kuwa “yeye ni kiongozi wa kitaifa na hafai kutuomba ruhusa akiwa na nia ya kututembelea mashinani”.
“Mimi sikuwa na ufahamu kwamba Bw Gachagua alikuwa atembee Mathioya siku hiyo,” Bw Mugo alisema.
Naye Bw Nyutu alisema kwamba kuna hali nyingine ambazo huwezi ukazificha kwa macho ya umma.
“Bw Nyoro anapendwa mashinani na tutamshikilia kwa vyovyote vile,” akasema Bw Nyutu.
Bi Maina kwa upande wake alisema kwamba kwa sasa “tunamsaidia mmoja wetu tunayempenda na ambaye ni Bw Nyoro kutimiza maendeleo hapa mashinani”.
Bi Maina ameolewa na mwandani wa Bw Gachagua ambaye ni mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi.
Miereka hii ya ubabe sasa inaonekana wazi kuvuruga masuala mengi hata yaliyo nje ya ulingo wa kisiasa.