Arsenal yapoteza matumaini ya Tottenham kuishikia Man City
NA MWANGI MUIRURI
MATUMAINI ya Arsenal kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kungoja kwa miaka zaidi ya 20 yako kwa kiwango kikuu ndani ya timu ya Tottenham Hotspur.
Lakini mchezo wa Spurs umedorora kiasi kwamba mnamo Alhamisi usiku, ilitandikwa mabao 2-0 na Chelsea, hali ambayo imewasononesha mashabiki wa Arsenal.
“Nilitarajia Spurs ionyeshe ari ya kuwa na tamaa ya kushinda mechi zake ndio imalize ndani ya mduara wa nne-bora. Katika tamaa hiyo ndipo sisi wa Arsenal tulikuwa na imani kwamba ingetusaidia kutwaa ligi lakini sasa inakaa tuko kivyetu,” akasema shabiki sugu wa Arsenal mjini Karatina, Stephen Kiaraho.
Mabao ya Chalobah na Jackson katika dakika za 24 na 72 mtawalia yalizamisha Spurs bila jibu.
Hii ni ikizingatiwa kwamba kwa sasa kinyang’anyiro hicho cha EPL msimu wa 2023/24 kimebakia kuwa kati ya Arsenal na Manchester City huku kukibakia mechi nne pekee mbivu na mbichi ibainike.
“Sisi tulikuwa tunatazamia Spurs watupe afueni kwa kutushikia Man City. Tunahitaji tu sisi tushinde mechi zetu zilizosalia nao Man City wapoteze mechi moja tu. Ikiwa ngumu zaidi, sisi tushinde mechi zilizosalia nao Man City watoke sare katika mechi moja tu,” akasema Seneta Maalum Karen Nyamu.
Kwa sasa Man City wako katika nafasi ya pili katika jedwali kwa pointi 79 Arsenal ikiongoza kwa 80.
Arsenal imebakisha udhia na timu za Bournemouth, Manchester United na Everton huku Man City ikisaka kuadhibu Wolves, Spurs, West Ham United na Fulham.
Iwapo Man City itashinda mechi zote iliyosalia nazo, itaibuka bingwa kwa mara ya sita mfululizo kwa pointi 91 huku ikiwa nayo Arsenal itashinda zote tatu itaibuka ya pili kwa pointi 89.
Iwapo Man City itashikwa kwa sare moja, nayo Arsenal ishinde zote zake, basi timu zote mbili zitamaliza ligi zikiwa na pointi 89 lakini ubora wa mabao utawaze Arsenal kuwa mabingwa.
Ilivyo kwa sasa, ni Man City ambayo ushindi wa mechi zake utaihakikishia ubingwa, Arsenal ikitarajia mikosi ya kujikwaa kwa vijana hao wa Pep Guardiola.
Timu ya Man City ilitangaza nia ya kuhepa na ubingwa Jumapili iliyopita ilipoinyuka timu ya Nottingham Forest kwa mabao mawili bila jibu.
Mashabiki wa Arsenal walikuwa wakitarajia Man City wajikwae angalau watoke sare au waadhibiwe lakini ikawa si hivyo.
Hata hivyo, huku Man City ikionekana kuwa na timu rahisi katika mechi zilizosalia, Arsenal inangojea kisiki kikuu ambacho ni Man United.
Man United hupenda sana kuadhibu Arsenal na mashabiki wake huwezi ukawapata wakiombea Arsenal ushindi au ubingwa wa aina yoyote.