Habari za Kaunti

Nyamira: Wafanyakazi 79 watolewa tonge mdomoni kwa kutumia vyeti feki

May 3rd, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

WAFANYAKAZI 79 wa serikali ya Kaunti ya Nyamira wanakabiliwa na hali mbaya ya kupoteza kazi na marupurupu mengine baada ya kubainika kuwa walitumia vyeti feki vya masomo kupata ajira na kupandishwa vyeo.

Kutokana na hali hiyo, gavana Amos Nyaribo amesema serikali ya kaunti imesitisha mara moja malipo ya mishahara yao.

Aidha amesema majina ya watu hao yametumwa kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yao.

Akihutubia wanahabari Ijumaa asubuhi katika makao makuu ya kaunti, Bw Nyaribo alisema huo ni msako wa kwanza unaolenga kusafisha mishahara ya kaunti kwa kuwaondoa watu wasio na sifa hitajika lakini wamekuwa wakijipatia mamilioni ya pesa kutoka kwa hazina ya kaunti.

“Nilitoa ahadi kwa watu wa Nyamira kwamba nitawalindia rasilimali zao, kuhakikisha uadilifu na kuiheshimu Katiba. Ili kulinda uadilifu wa orodha yetu ya mishahara na Utumishi wa Umma, Serikali ya Kaunti ya Nyamira ilifanya mchakato wa kukagua vyeti vya masomo vya wafanyakazi wetu,” Gavana Nyaribo akasema.

Aliongeza, “Katika mchakato wa kwanza, jumla ya vyeti 2,821 vya KCSE viliwasilishwa kwa Baraza la Mitihani ya Kitaifa Nchini (KNEC). KNEC iliwasilisha ripoti kwetu Aprili 2024 ikionyesha tofauti ya alama za wastani kwa baadhi ya vyeti. Katika baadhi ya matukio, nambari za usajili wa mitihani (index numbers), hazikuwa za maafisa wetu.”

Alisema majina megine kwenye vyeti hivyo yalikuwa yameghushiwa.

Kulingana na Bw Nyaribo, Idara zilizoathiriwa ni pamoja na Afya (kesi 24), Fedha na Usimamizi wa Utumishi wa Umma (kesi 13 kila mojawapo), Ofisi ya Gavana na Ardhi (kesi tisa kila moja), Elimu na Mazingira (kesi tatu kila moja), na Jinsia, Biashara na Bodi ya Utumishi wa Umma (kesi moja moja).

Gavana Nyaribo pia alibainisha kuwa katika tapo la pili la vyeti vya masomo litawasilishwa kwa KNEC na vyuo vya kiwango cha kati wiki ijayo ili kuthibitishwa.

Mbali na hayo, gavana Nyaribo alisema kuwa baadhi ya watumishi 245 walitumia udanganyifu kupandishwa vyeo lakini hivi karibuni ripoti yao itadhihirika.

“Kuna mtu mmoja ambaye alijipandisha cheo baada ya siku moja tu. Hatutawaacha watu kama hao,” Bw Nyaribo alisema.

Kulingana na gavana Nyaribo, wafanyakazi 79 ambao mishahara yao ilisitishwa wamekuwa wakipokea Sh48 milioni kila mwezi.

Baadhi ya watumishi ambao mishahara yao imesimamishwa wanashikilia nyadhifa za juu serikalini.

Mnamo Mei 2023, gavana Nyaribo alipotangaza kuanza kwa ukaguzi wa wafanyakazi, maafisa wawili wakuu kutoka Idara ya Nguvukazi (HR) walikamatwa na DCI kwa matumizi mabaya ya ofisi.

Washukiwa hao walikabiliwa na mashtaka ya uhalifu unaohusiana na shughuli mbalimbali ambazo zilidaiwa kusababisha wizi wa rasilimali za kaunti kwa njia za kutiliwa shaka.