Makala

Aliyetupwa jela akiwa na malaria ya ubongo aachiliwa

May 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA TITUS OMINDE

BAADA ya kutumikia kifungo cha miaka 36 gerezani kwa kupatikana na hatia ya mauaji licha ya kutatizika kiakili kwa malaria ya ubongo, Philip Kemboi Bor hatimaye ameachiliwa huru.

Mwanamume huyo alifungwa akiwa na umri wa miaka 18 mnamo mwaka 1989.

Bw Bor ambaye aliachiliwa mnamo Alhamisi akiwa na umri wa miaka 54 ana kila sababu ya kusifia Katiba ya mwaka 2010 iliyoanza kufanya kazi kikamilifu mwaka 2013.

Kupitia ushauri wa wakili wake Oscar Oduor wa kutoka Kituo cha Usaidizi wa Kisheria na Urekebishaji wa Wafungwa (CELSIR), Bw Bor alikata rufaa mwaka wa 2019.

Mahakama ilimwachilia Bw Bor kwa kuzingatia kifungu cha 166 cha kanuni za adhabu.

Bw Bor aliridhisha Jaji Reuben Nyakundi kwamba alistahili kupata uhuru kutoka kwa minyororo ya jela lakini kizuizi cha kipekee kati yake na uhuru wake, kilikuwa ripoti ya uchunguzi wa kiakili ili kubaini ikiwa sasa yuko sawa kiakili.

Mnamo Aprili 22, 2024, Bw Bor alipata ripoti kuhusu akili yake ambapo matokeo yalikuwa ya kumpa tabasamu.

Ripoti hiyo kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) ilibaini kuwa alikuwa na akili timamu.

Baada ya kupokea ripoti hiyo, jaji Nyakundi aliendelea na kutoa amri ya kuachiliwa ambayo ilimfanya Bw Bor kutoka gerezani baada ya kutumikia kifungo cha miaka 36 jela.

Bw Philip Kemboi Bor ambaye alifungwa akiwa na umri wa miaka 18 mwaka wa 1989. Gazeti la Daily Nation liliangazia uwezekano wa kuachiliwa kwake wiki mbili zilizopita. PICHA | TITUS OMINDE

Punde tu baada ya kuachiliwa Bw Bor alifika katika duka la kuuza nguo mjini Eldoret ambapo alipata suti mpya ya kijani kibichi kwa hisani ya CELSIR.

Taifa Leo ilikutana naye katika ofisi ya wakili wake iliyoko katika jengo la Meadows, kwenye barabara ya Elgeyo, ambapo alikuwa ameenda kumshukuru wakili wake–Bw Oduor na wafanyakazi wote wa CELSIR–akisifia ukarimu wao hasa kwa suti mpya na jozi mpya ya viatu.

“Nimejifunza mengi nikiwa gerezani na ninaenda kujenga kwetu nyumbani. Ninatumai kuoa na maisha yaendelee,” akasema Bw Bor.

Mfungwa huyo aliyeachiliwa huru alisema anawazia kuwa mhubiri.

Bw Philip Kemboi Bor (kushoto) akiwa na wakili wake Oscar Oduor mara baada ya kuachiliwa kutoka gerezani baada ya kutumikia kifungo cha miaka 36 jela alipopatikana na hatia lakini akiwa na matatizo ya malaria ya ubongo. PICHA | TITUS OMINDE

Mnamo Februari 26, 1988, alikuwa akipata nafuu kutokana na ugonjwa wa malaria wa ubongo.

Ilidaiwa kwamba akiwa usingizini, jirani yake alimwamsha na kwa kushtuka na kugutuka, akampiga jirani huyo ambaye baadaye alizimia na kuaga dunia.

Kufuatia tukio hilo, alikamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi cha Lesos, Kaunti ya Nandi.

Kwa sababu ya hali yake ya akili, hakuweza kujibu maswala yaliwasilishwa kwake kutokana na kesi hiyo.

Alidai kuwa kutokana na hali yake ya akili alipigwa huku akituhumiwa kukataa kujibu masuala ambayo alikuwa akihojiwa kutokana na mauaji husika.

Kufuatia hali yake, alipelekwa katika MTRH mjini Eldoret kwa matibabu ya majeraha aliyopata wakati wa kukamatwa na baadaye kuwasilishwa kortini kujibu mashtaka ya mauaji mnamo Machi 3, 1988.

Julai 7, 1989, marehemu Jaji Daniel Aganyanya alimpata na hatia ya mauaji licha ya kuwa na kichaa.

Baadaye alifungwa kusubiri radhi ya Rais.