Raila Odinga: Ningekuwa Rais ningeokoa Kenya kutoka kwa matatizo yanayotukumba saa hii
NA LABAAN SHABAAN
KIONGOZI wa Upinzani Raila Odinga amesema ni yeye angeokoa Kenya iepuke matatizo yanayokumba nchi sasa.
Alizungumza muda mfupi baada ya Rais William Ruto kuhutubia taifa kuhusu utayarifu wa kukabili janga la mafuriko ambalo linatarajiwa kuzidi kuathiri nchi.
Kiongozi huyo wa Muungano wa Azimio la Umoja – One Kenya alidai kuwa serikali ina mawaziri ambao ni watepetevu kazini na hawaelewi jinsi ya kuendesha nchi.
“Sisi tuna shida na sisi kama Azimio tuna suluhu. Tungekuwa kwenye serikali tusingekuwa na shida hizi,” alisema Bw Odinga akiwadunisha mawaziri Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani), Susan Nakhumicha (Afya), Mithika Linturi (Kilimo), Ezekiel Machogu (Elimu).
“Tuna shida kwa sababu tuna dereva lakini hajui usukani uko wapi.”
Kiongozi wa chama cha ODM alikuwa akihutubia wakazi wa Embakasi Kusini, Nairobi alipopinga amri ya Wizara ya Usalama kuongoza ubomozi wa nyumba zilizojengwa katika ardhi ya chemchemi ya maji mtaa wa Mukuru kwa Ruben.
Bw Odinga anataka serikali iwajengee makazi kabla ya kuwabomolea nyumba zao.
“Kwanza wajengeeni nyumba kabla ya kuwaharibia makazi. Wakenya si wanyama na lazima muwe na nyoyo za utu,” akasema.
Kadhalika, Bw Odinga alimkashifu Waziri Machogu kwa kutoa tangazo la kuahirisha ufunguzi wa shule usiku wa manane, tukio ambalo liliwasababishia washikadau wa elimu masumbufu makubwa.
“Walisema shule zingefunguliwa lakini walisubiri hadi dakika ya mwisho baada ya wanafunzi kurejea shuleni kisha wakatangaza shule hazifunguliwi,” alifoka.
Rais Ruto, hata hivyo, Ijumaa alitangaza kwamba shule hazitafunguliwa mpaka mwongozo mpya utolewe.