Dimba

Eti Arsenal kwa asilimia 64 itanyuka Man U mnamo Mei 12

May 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI 

MNAMO Mei 12, 2024, kuanzia saa kumi na mbili na nusu jioni, Arsenal watakaribishwa na mahasimu wao wa jadi Manchester United ugani Old Trafford kwa mtanange wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mashabiki wa klabu hizo mbili wanasema mechi hiyo ni sawa na kisa cha mwaga ugali nimwage kitoweo.

Utakuwa mchezo wa maana kwa timu zote mbili ambapo Arsenal ikisaka ubingwa wa EPL uliowahepa kwa zaidi ya miaka 20 sasa, Manchester United itakuwa ikisaka kufuzu kwa saba-bora ili kujiweka kwa nafasi ya kushiriki katika mojawapo ya dimba za Europa.

Kwa sasa, Arsenal inaongoza jedwali kwa pointi 80 ikifuatwa na Manchester City iliyo na pointi 79.

“Shida ya mechi hii ni kwamba Man U na Arsenal huwa hawatekelezi undugu wa ushabiki. Ni timu ambazo hutaniana kiasi kwamba mmoja akimshinda mwingine, huonekana kama ufanisi wa Karne moja ijayo,” asema aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi ambaye ni mfuasi wa Arsenal.

Bw Ngugi anasema kwamba mtanange huo utakuwa wa kufa kupona kwa kuwa Arsenal ikiponyoka na ushindi na Man City iwe imeteleza, basi Arsenal itatwaa ubingwa wa EPL.

“Mambo yakienda mrama na Man U itamalaki kwa kila safu, basi itakuwa katika nafasi bora kumaliza ndani ya saba-bora. Afadhali sasa iwe ni sare ndio hata tukipoteza malengo yetu ya msimu kwa hali ilivyo sasa, kusiwe na wa kukejeli mwingine,” asema Bw Ngugi.

Hata hivyo, ni vyema ieleweke kwamba Man U inashindana na Newscastle, West Ham United na Chelsea kumaliza ndani ya saba-bora.

Kwa upande wake, Arsenal kwa raha zake imejiweka katika nafasi bora ya kumaliza ndani ya nne-bora na kujihakikishia kushiriki dimba la Klabu Bingwa Ulaya (Uefa) msimu ujao.

“Kile kinachotusumbua kwa sasa ni ubingwa wa EPL ambapo ili tuutwae, ni lazima tushinde mechi zetu tatu zilizosalia zikiwa ni kati ya Bournemouth, Man U na Fulham,” asema Seneta Maalum Karen Nyamu.

Hata hivyo, Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, ambaye ni shabiki sugu wa Man U, anasema kwamba “sijalishwi na timu ndogo kama Arsenal” na nia ya Mashetani Wekundu, yaani The Red Devils kama wanavyojiita Man U, ni kushinda mechi zote zilizosalia.

“Kwa sasa nia yetu ni kupata pointi zote 12 zilizosalia. Hilo litatuweka popote pale ambapo hatujali ni wapi. Bora tu tupige Arsenal sisi tuko sawa,” akasema Bw Nyoro.

Hata hivyo, udadisi wa takwimu za EPL unaonyesha kwamba Arsenal kwa kiwango cha asilimia 64, itaishinda Man U.

Nayo Man U imepewa ubashiri wa ushindi kwa asilimia 17, uwezekano wa sare ukiwa asilimia 19, hali ambayo Bw Nyoro ameitaja kama “ndoto ya kipuuzi kwa kuwa liwe liwalo, Arsenal italia sana pale Old Trafford”.