Maambukizi ya kipindupindu yaongezeka mafuriko yakiendelea
NA ANGELA OKETCH
NCHI imerekodi visa 34 vya kipindupindu, vinavyohusishwa na mafuriko huku mvua kubwa ikiendelea kushuhudiwa katika kaunti mbalimbali nchini.
Katibu katika Wizara ya Afya, Bi Mary Muthoni, alisema kuwa baadhi ya vyoo vimeporomoshwa na mafuriko, jambo ambalo limefanya maji machafu kutiririka hadi kwenye vyanzo vya maji.
Visa hivyo vimeripotiwa katika Kaunti ya Tana River huku Garsen Magharibi ikiripoti kesi 32 na Garsen ya Kati ikiripoti visa viwili.
Hata hivyo, Bi Muthoni alisema kuwa baadhi ya serikali za kaunti hazijaripoti visa vya kipindupindu kwa wizara ya afya.
Kipindupindu mara nyingi huhusishwa na mazingira machafu.
Mvua inayoendelea kunyesha nchini ni kero kubwa kwani huenda ikafanya maambukizi ya ugonjwa huo kuongezeka kwa kasi.
Kando na ugonjwa wa kipindupindu, visa vya ugonjwa wa kuhara pia vimeripotiwa katika kaunti ya Marsabit.
“Vyanzo vya maji vilivyochafuliwa vinaingia kwenye nyumba za watu na kuhangaisha jamii na hivyo kuongeza hatari ya magonjwa yanayosababishwa na bakteria kusambaa. Hatua za haraka zinahitajika ili kupunguza athari za mlipuko huu na kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo,” Bi Muthoni alisema.
Kulingana na Bi Muthoni, chanzo kikuu cha maambukizi ya kipindupindu kinaonekana kuwa vyanzo vichafu vya maji, ikichangiwa na ukosefu wa usafi wa mazingira katika maeneo yaliyoathiriwa. Juhudi zinaendelea kubaini na kukarabati vyanzo hivyo ili kudhibiti msambao wa ugonjwa huo hatari.
“Iwapo uko katika eneo lisilo na maji, kuna hatari unaweza kula chakula bila kunawa mikono hivyo kuambukizwa ugonjwa wa kipindupindu,” Bi Muthoni alisema.
“Japo tunajaribu kukabiliana na hali hiyo, mvua kubwa inayoendelea kunyesha na mafuriko inafanya mambo kuwa mabaya zaidi.”
Katika kukabiliana na mlipuko huo, kampeni za afya ya umma zimezinduliwa ili kuongeza ufahamu kuhusu jinsi ya kuzuia kipindupindu na umuhimu wa kanuni za usafi wa mazingira.
Wanajamii wanashauriwa kuchemsha au kutumia maji safi ya kunywa, kufanya mazoezi ya kunawa mikono mara kwa mara, na kutafuta matibabu ya haraka ili kubaini dalili za kipindupindu.
“Tunatoa vifaa vya dharura kusaidia katika usimamizi wa wagonjwa huku tukisambaza vifaa vya kusaidia kusafisha vyanzo vya maji na kutibu maji katika maeneo yote hatari,” alisema katibu huyo.