Murang’a Seal yalazwa kwao ‘kejani’ 3-1 na K’Ogalo
Na MWANGI MUIRURI
KLABU ya Gor Mahia kinyume na adabu za mgeni mnamo Jumamosi, imezuru Kaunti ya Gavana Irungu Kang’ata kuvaana na Murang’a Seal na ikaacha huko kilio cha mwenyeji kupigwa 3-1.
Mechi hiyo ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu nchini Kenya (FKF-PL) ilichezewa katika uga wa St Sebastian Park almaarufu Shakahola na ambao ndio nyumbani kwa Murang’a Seal.
Mchezaji Austin Odhiambo aliiweka Gor Mahia kifua mbele katika dakika ya nne kabla ya John Kiplagat kuisawazishia Seal kunako dakika ya 34. Lakini mabao mawili ya Benson Omalla katika dakika za 76 na 90+4 zilizika wenyeji katika uga huo wao wa Shakahola.
Uwanja huo wa mwekezaji wa kibinafsi anayejulikana kama Robert Macharia na ambaye ni wakili kitaaluma, pia hufahamika kama SportPesa Arena na jina Shakahola lilisukwa na wenyeji wa Murang’a kutokana na umbali wake ndani ya kichaka ambapo kutoka mjini, wahudumu wa pikipiki hulipisha mashabiki nauli ya Sh300 ili kuufikia.
Aidha, barabara ya kuelekea katika uwanja huo huwa na ukatili wake kwa kuwa ni nyembamba kando, ikizingirwa na vichaka na pia kwa msimu huu wa mvua, ikijaa maji na matope.
Kocha wa Murang’a Seal Juma Abdallah ambaye kabla ya mechi hiyo alikuwa amesisitiza hakuwa akiogopa timu hiyo ya Gor, aliingia mitini baada ya matokeo kuthibitishwa kwa kipenga cha mwisho kutoka kinywa cha refa.
Ligi hiyo ya timu 18 kwa sasa inaongozwa na Gor kwa pointi 60 ikifuatwa na Kenya Police iliyo na pointi 48 huku Tusker wakiwa wa tatu kwa pointi 46. Murang’a Seal ni ya 11 kwa pointi 35.