Wakazi Lamu waona faida za njia za cabro walizodharau
NA KALUME KAZUNGU
MWAKA 2013 Gavana wa kwanza wa Kaunti ya Lamu, ambaye pia ndiye anayekalia kiti kwa sasa, Bw Issa Timamy, alifichua ndoto yake kuihusu miji mikuu ya eneo hilo kwamba ijengwe vizuri na njia au barabara za miji hiyo ziwekwe cabro.
Ili kufanikisha hayo, Bw Timamy akazindua mradi wa kwanza wa ujenzi wa cabro kwenye Mji wa Kale wa Lamu.
Ni hatua ambayo ilileta bezo na kejeli tele, baadhi ya wakazi wakimbandika jina ‘Gavana wa ma-Cabro’.
Kila walipopata nafasi kukutana, wananchi na wapinzani wa mwanasiasa huyu walipiga gumzo uliojaa mzaha kwamba Bw Timamy hana miradi mingine yoyote ya maanda eneo hilo ila kuwekea wananchi wanyonge cabro.
Zaidi ya miaka 10 baadaye, bezo hizo za awali kwa sasa zimegeuka kuwa raha na baraka tele kwani miji karibu yote mikuu ya Lamu na hata vijibaraste vyake vinameremeta kwa kujengewa njia za cabro.
Unapotembea kwenye Mji wa Kale wa Lamu, ule wa Mokowe, Mpeketoni, Faza, Witu, Kizingitini, na hata Kiunga iliyoko mpakani mwa Kenya na Somalia, utafurahia na moyo kuridhika unapotembea kwenye njia za cabro.
“Najua kuna wanaokereka wakisikia nikiendelea kutoa ahadi zangu za kuweka cabro kwenye baadhi ya njia za miji ya Lamu. Hata kuna wanaoniita mimi kuwa Gavana wa ma-Cabro. Nataka kuwaambia kuwa nimekubali jina hilo. Nitaendelea kujenga hizi cabro kila upande wa Lamu ilmradi maisha ya watu wetu yaboreke,” akasema Bw Timamy.
Baadhi ya wakazi waliohojiwa na Taifa Jumapili hawakuficha furaha yao kutokana na juhudi za Gavana Timamy kuwajengea cabro kwenye miji yao.
Bi Fatma Aboud, mkazi wa kisiwa cha Faza, anasema tangu cabro ziwekwe mjini humo, usafi umeimarika vilivyo.
Bi Aboud aliutaja mradi huo kuwa wa maana kwani pia matembezi yao mjini yamekuwa rahisi.
“Njia za mji wetu zilikuwa ni za mchanga tu ambapo kutembea si rahisi. Tangu cabro ziwekwe, matembezi yamekuwa rahisi na usafi wa mji umeboreshwa hata zaidi,” akasema Bi Aboud.
Naye Bw Said Aboubakar, ambaye ni mkazi wa Mji wa Kale wa Lamu, alisema kuwepo kwa cabro mjini humo kumewavutia watalii kuzuru eneo hilo kila mara.
Bw Aboubakar alisema miaka ya awali, watalii walikuwa wakilalamikia hali ya usafi kwenye mji wa kale ambayo ilikuwa duni.
“Kabla hizi cabro mpya kuwekwa na Gavana Timamy kwenye mji wetu, watalii wengi walikuwa wakisusia kutembea hapa kwa sababu kuwa mji ni mchafu. Twashukuru kuwepo kwa cabro kumeipa Lamu taswira ya kupendeza, hivyo kuwavutia watalii wengi kufika hapa,” akasema Bw Abounakar.
Wakazi pia walitaja kwamba kuwepo kwa muundimsingi huo kumepiga jeki mipangilio ya miji mingi ya Lamu.
Bw Simon Mungai, mkazi wa mji wa Mpeketoni, alisema kila anayezuru mji huo miaka ya hivi karibuni amejionea mwenyewe jinsi mpangilio ulivyoimarika kutokana na kuwepo kwa cabro.
Bw Mungai alisema cabro pia zimesaidia kuelekeza maji chafu kunakofaa kila kunaponyesha mvua kinyume na awali.
“Zamani mji kama Mpeketoni ulikuwa ukisheheni vidimbwi vya maji chafu kila kunaponyesha. Tangu tuwekewe cabro, hilo hatulishuhudii tena,” akasema Bw Mungai.
Aliongeza, “Hizi cabro zimeimarisha mipangilio ya miji mingi Lamu. Si Mpeketoni, si Witu, si Faza… miji imepewa surya mpya na ya kuvutia kabisa kwa macho. Hata vijana wetu wa bodaboda sasa wanafurahia kuwepo kwa cabro. Kumerahisisha mizunguko yao mjini.”
Wananchi pia wameupokea mradi wa cabro kwa mikono miwili, wakisema umesaidia kupunguza uhalifu kwenye baadhi ya miji ambayo awali ilishuhudia wizi.
“Hata wezi wanaogopa kuiba wakijua fika kuwa watakimbizwa na kushikwa rahisi. Njia za cabro ni rahisi mwizi kukimbizwa na kushikwa,” akasema Bw Kamau Mbuthia.
Wakazi aidha walimuomba Bw Timamy kuzingatia pia kuweka cabro kwenye miji midogo ya Lamu, ikiwemo Hindi, Mkunumbi, Koreni, Mapenya, Bar’goni, Magogoni na kwingineko.
“Mahali kama hapa Hindi twahitaji cabro zitandazwe. Mvua inaponyesha huwa kuna changamoto ya mafuriko. Ninaamini hizi cabro zikiwekwa hali itapungua,” akasema Bi Sicilia Kinuthia ambaye ni mfanyabiashara mjini Hindi.