Habari za Kitaifa

Mahangaiko ya wasafiri katika barabara ya kuunganisha Kenya na Sudan Kusini

May 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA OSCAR KAKAI

MAMIA ya wasafiri wamekwama kati ya eneo la Lous na Kambi Karai, kaunti ya Pokot Magharibi kwenye barabara kuu ya Kitale-Kapenguria-Lodwar-Juba kwa siku tatu baada ya kukatika kwa sababu ya mafuriko.  

Uchukuzi umeathirika na biashara kuharibika kwenye barabara hiyo kuu ya kipekee ambayo inatoka Trans Nzoia, kufululiza hadi Pokot Magharibi, Turkana na kisha nchini Sudan Kusini.

Taifa Leo ilijionea magari ambayo yamejipanga kwenye foleni yakiwa yamekwama kwenye barabara hiyo.

Magari hayo ni malori ya trela na matatu za uchukuzi wa abiria.

Aidha, abiria wako barabarani wakisubiri njia mbadala iweze kupitika.

Hali hii imeathiri usafiri wa abiria na uchukuzi wa bidhaa huku nauli ikiongezeka maradufu na wasafiri kupoteza muda mwingi na kupata hasara.

Dereva Dennis Oboy aliyekuwa ametoka Kaunti ya Bungoma ambaye alikuwa anaelekea mjini  Lodwar na kukwama kwenye barabara hiyo, anaitaka Halmashauri ya Barabara Kuu Nchini (KeNHA) na shirika la Kenya Red Cross kuingilia kati na kuharakisha ukarabati wa barabara hiyo.

“Nimekuwa nikitumia barabara hii kwa miaka 20 sasa kutafuta riziki lakini mara hii sasa mambo yameharibika. Tumekaa hapa kwa siku mbili sasa na tukifika eneo la Lochwaa tutakaa siku zaidi,” akasema Bw Oboy mnamo Jumamosi.

Alisema kuwa pia wameathirika na kafiu katika eneo la Kainuk.

“Huwezi kupita eneo la Marich ikifika saa 12 jioni ikiwa umebeba mizigo. Njia mbadala ambayo inawekwa ni telezi,” akasema.

Bw Evans Onyango, msafiri kutoka Kaunti ya Trans-Nzoia ambaye alilala eneo la Lous alilalamikia kuishi muda mrefu kwenye barabara.

“Sina chochote na ninafaa kurudi nyumbani kuangalia familia yangu,” alisema Bw Onyango.

Alielezea ghadhabu kwa kile alidai ni kusahaulika na serikali baada ya barabara hiyo kukatika.

Alisema kuwa kuchelewa huko huwaletea hasara kubwa.

“Bidhaa zetu zimeharibika. Magari yameharibika na matumizi yamepanda juu,” alisema.

Bi Florence Manyonge, mwalimu kutoka Kaunti ya Turkana ambaye alisafiri kutoka mjini Lodwar, anashangaa ni kwa sababu gani barabara hiyo haijatengenezwa kutoka Jumanne wiki jana.

“Nilianza safari saa kumi na moja asubuhi lakini hadi sasa bado niko hapa. Tulikuwa tumesafiri wiki jana kuenda shuleni lakini serikali imebadilisha siku ya kufungua shule. Tuko na watoto hapa wanalia sababu ya njaa na hakuna duka hapa. Tumekwama na huwezi kuenda Kitale ama Lodwar. Hakuna polisi na maafisa wa Red Cross hapa,” alisema Bi Manyonge.

Mwalimu mwingine ambaye alijitambulisha kama Bi Wepukhulu kutoka eneo la Mlima Elgon ambaye anafunza eneo la Lokichogio, kaunti ya  Turkana, aliisuta serikali kwa kupeleka walimu sehemu za mbali ambapo kuna barabara mbovu.

“Tuko na njaa na hata mume wangu amechoka na amelala msituni. Tunahitaji msaada sababu sisi hulipa ushuru. Tulianza safari saa nane usiku kutoka Lokichogio,” akasema Bi Wepukhulu.

Naye Bw John Lukuk, mkazi wa eneo hilo alisema kuwa nauli imepanda na wasafiri wanalazimika kulipa fedha zaidi.

Alisema kuwa hali hiyo ni pigo kubwa kwa uchumi wa eneo hilo sababu biashara na usafiri zimeathirka.

“Wafanyabiashara wanachelewa barabarani na bidhaa,” alisema.

Alitoa wito kwa serikali kuwasadia na kuharakisha ukarabati wa barabara hiyo ili watu na bidhaa kuweza kupita.

KeNHA inapambana kutengeneza njia mbadala kuimarisha usafiri.

[email protected]