Korti yakataa kuzima kesi za ushuru wa nyumba, yaamuru majaji sita wasikize zote
NA JOSEPH OPENDA
KESI sita zinazopinga mradi wa nyumba za gharama nafuu unaovumishwa na Rais William Ruto, sasa zitasikizwa na zaidi ya majaji watatu.
Hii ni baada ya mahakama kukatalia mbali ombi la serikali kuwa kesi hizo zitupwe.
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Hazina Kuu Kifedha na Mwanasheria Mkuu ilikuwa imewasilisha ombi ikitaka kesi hizo zilizowasilishwa na watu tofauti na makundi isisikizwe na zitupiliwe mbali.
Kupitia ombi lake, serikali ilikuwa imesema kuwa mahakama haifai kisheria kusikiza kesi hizo, walioziwasilisha walikosa kufuata mkondo wa kisheria unaohitajika na pia hawakunukuu hasa ni haki za zipi ambazo zilikuwa zimekiukwa.
Hata hivyo, Jaji Chacha Mwita kwenye uamuzi wake alipuuzilia mbali ombi hilo na akaamrisha kesi hizo sita ziunganishwe na kusikizwa pamoja. Jaji huyo aliwasilisha suala hilo kwa Jaji Mkuu Martha Koome ili ateue jopo la majaji saba ambao watasikiza na kuamua kesi hizo.
Jaji Mwita alikubaliana na waliowasilisha kesi hiyo kuwa hoja walizoibua zinahusiana na uhalali wa kisheria wa mpango huo na zinastahili kusikizwa na zaidi ya jaji moja.
“Kuna madai kuwa katiba ya Kenya imekiukwa katika baadhi ya hoja ambazo zimewasilishwa. Haya ni masuala mazito pamoja na lile kuwa mpango huo unastahili kuendeshwa na utawala wa kaunti au serikali kuu,” akasema Jaji Mwita.
Jaji huyo aliongeza kuwa korti ina mamlaka ya kusikiza na kuamua kesi iliyowasilishwa kinyume na madai ya asasi hizo za serikali. Asasi hizo zilikuwa zimedai kuwa kesi hiyo inastahili kusikizwa na kuamuliwa na Mahakama ya Mazingira na Ardhi kwa sababu inazungumzia masuala ya nyumba na ardhi.
Kesi hizo sita ziliwasilishwa tarehe tofauti baada ya Rais William Ruto kutia saini Sheria ya Nyumba za gharama nafuu 2024 baada ya mswada huo kupitishwa na bunge.
Waliowasilisha kesi hizo sita ni Seneta wa Busia Okiya Omtata, raia Moses Nthurima Pauline Nduta, Philemon Abuga, Jamlick Otondi na Shalom Kaka.
Wengine Benjamin Magare ambaye ni daktari wa Nakuru, Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu na Taasisi ya Katiba. Walishtaki wizara za ardhi, hazina kuu ya kifedha, mwanasheria mkuu, bunge la kitaifa na seneti.
Kesi nyingine ambayo pia iliwasilishwa majuzi na Peter Okiro ilihamishwa hadi Nakuru. Bw Okiro mnamo Machi 25 alisema sheria hiyo ni haramu na ni kinyume cha katiba.
Kupitia wakili wake Kipkoech Ng’etich, Bw Okiro alisema vifungu vya sheria vinavyowalazimisha Wakenya wachangie mradi huo vinakiuka hali yao ya kumiliki mali.
“Serikali imetupa katiba kwenye kaburi la sahau na inatumia bunge vibaya kupitisha sheria zinazowaumiza Wakenya,” akasema Bw Okiro.
Kesi zote ambazo zimeunganishwa zitasikizwa mnamo Mei 16.